Wastaafu wa iliyokuwa EAC sasa waokota ‘makopo’ Dar

Baadhi ya wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waliofanya makazi kuwa nje ya uzio wa eneo la TRC wakiendelea na shughuli za kila siku katika makazi yao. (Picha na Joachim Mushi)

BAADHI ya Wazee Wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) sasa wamegeuka waokota makopo na chupa jijini Dar es Salaam, wakitafuta fedha za kujikimu.

Uchunguzi uliofanywa na dev.kisakuzi.com jijini Dar es Salaam kwa muda, umebaini wazee hao sasa wanaokota makopo na chupa katika mitaa kadhaa ya jiji la Dar es Salaam (hasa katikati ya jiji) wakitafuta vijisenti vya kuweza kuishi ndani ya jiji.

Wazee hao ambao bado wanavutana na Serikali ya Tanzania kwa madai kadhaa zikiwemo stahili za kustaafu kwao, wanakusanya chupa na baadhi ya makopo na kuyauza kwa wahitaji na kupata fedha za kujikimu.

Aidha wazee hao wameamua kuhamia nje ya uzio wa Stesheni ya treni iliyopo karibu na Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam na kufanya eneo hilo makazi ya kudumu na wamekuwa wakilala nje baadhi yao kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Akizungumza na dev.kisakuzi.com mmoja wa wazee hao, John Kizito aliyetokea Mwanza tangu 2003, amesema kwa sasa wao wanaishi kwa matumaini, hawaijui kesho wala leo inapita vipi. “Sisi kwa sasa ni kama boti lililopoteza muelekeo, yeyote aweza kutufanya atakavyo…kila kiongozi anayekuja anatuendesha atakavyo, fedha tunazodai hatupewi wala hawajui baadhi yetu bado tunaishi kwa shida hapa,” alisema Kizito ambaye alikuwa ameajiriwa kama baharia wa Mv. Victoria enzi za EAC (1972-78).

Naye Jumanne Sanane alisema jumla ya wazee 17 ndio walioweka makazi yao eneo hilo na wengine wamepanga ‘uswailini’ kulingana na uwezo wao, huku wakiangaika kama wao. Sanane ambaye alikuwa fundi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC-1967-2003) kituo cha Itigi amesema wanaishi kwa shida jijini Dar es Salaam hivyo wengine kuzunguka kama vichaa wakiokota makopo na chupa na kuuza ili wapate chochote.

“Juzi mmoja wetu kagongwa na bajaj akizunguka kuokota chupa mitaani na aliumia lakini, hatuna namna lazima tuendelee kuishi kwa shida hadi tutakapo fanikiwa, wapo wanaokufa na tunawaona…huenda siku moja tutafanikiwa dhidi ya madai yetu,” anasema mzee huyo.

mua kukaa kimya