Wasomi UDSM waikosoa bajeti ya elimu ‘live’

Wadau anuai wa elimu wakifuatilia kwa makini hotuba ya Dk. Shukuru Kawambwa ‘live’ kabla ya kuanza kutoa maoni yao katika mjadala leo Dar es Salam.

Kutoka kushoto ni Meneja Kitengo cha Habari wa HakiElimu, Nyanda Shuli, Mhadhiri Adolf Mkenda kutoka Idara ya Uchumi ya UDSM Mhadhiri wa UDSM, Dk. Kitila Mkumbo

Mhadhiri mwenzao kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano, Ayoub Rioba, akizungumza katika mjadala huo.

Na Joachim Mushi, dev.kisakuzi.com

TAASISI ya HakiElimu leo jijini Dar es Salaam imewakutanisha baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), walimu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu ambapo waliishuhudia bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Elimu ikiwasilishwa ‘live’ mjini bungeni mjini Dodoma kabla ya kutoa maoni yao.

Wadau hao wa elimu kwa pamoja waliishuhudia kupitia king’amuzi bajeti ya Wizara ta Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikiwasilishwa ‘live’ wakiwa kwenye mkutano kisha baadaye kutoa maoni yao jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa kuwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2012/13, Mhadhiri wa UDSM, Dk. Kitila Mkumbo alisema ameshangaa bajeti hiyo kutouona mgomo wa walimu wa juzi pamoja na migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kama ni tatizo kwa elimu na kuiingiza kama changamoto.

“Binafsi kati ya vitu ambavyo vimenishangaza ni bajeti hiyo kutotaja mgomo wa walimu katika bajeti iliyopita kuwa ni miongoni mwa changamoto za wizara hiyo…na hata migomo ya vyuo vikuu,” alisema Dk. Mkumbo alipokuwa akijadili katika mkutano huo.

Baadhi ya maofisa kutoka taasisi ya HakiElimu wakifuatilia mjadala huo


Alisema wizara imetaja kufanya vizuri katika elimu upande wa msingi na sekondari kwa kidato, lakini imekwepa kutoa mafanikio kwa kidato cha tano na sita eneo ambalo limefanya vibaya kwa matokeo ya hivi karibuni. Alikosoa kiwango cha uwiano kati ya wanafunzi na walimu kilichotatolewa kwa sasa (1:46) kwani idadi kubwa ya walimu wapo shule za mjini huku hali mbaya ikiwa vijijini.

Aidha aliongeza kuwa wizara pia imeshindwa kuona migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu ya mara kwa mara ni changamoto hivyo kushindwa kueleza katika bajeti yake. “…karibu asilimia 80 ya migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu imesababishwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, lakini hili halikutajwa katika bajeti ya waziri,” alisema msomi huyo.

Kwa upande wake Mhadhiri Adolf Mkenda kutoka Idara ya Uchumi ya UDSM akizungumza katika mkutano huo alisema bajeti iliyowasilishwa ni ya kawaida hivyo ni vigumu kumaliza changamoto lukuki za elimu zinazoikabili wizara hiyo.

Mhadhiri wa UDSM, Dk. Kitila Mkumbo akiwasilisha mada kabla ya mjadala huo


Alisema bajeti imejivunia ongezeko la idadi ya vyuo vikuu lakini imeshindwa kuonesha ubora wa vyuo hivyo jambo ambalo ni hatari endapo litaachwa, bila udhibiti. “…Twaweza kuwa na vyuo vingi lakini suala la ubora ni tatizo lingine. Pia uandikishaji wa idadi kubwa ya wanafunzi unatakiwa kulinganishwa na waliokusudiwa kuandikishwa…maana twaweza jivunia kiwango kinapanda kumbe tunadanganywa na ongezeko la idadi ya watu,” alisema msomi huyo.

Akizungumza kwenye mjadala Meneja wa Kitengo cha Habari wa HakiElimu, Nyanda Shuli alisema Serikali haiwezi kufanikisha elimu bora bila kuaandaa walimu bora katika utoaji wa elimu husika. “Huwezi kutegemea elimu bora pasipo na walimu bora, binafsi sijaona mkakati wowote mahususi wa kuboresha elimu,” alisema Shuli.

Ameishauri wizara ya elimu kujiandaa vizuri kimipango kabla ya kutekeleza mpango wa kuwa na shule ya kidato cha tano na sita kwa kila tarafa ili kuepuka madudu yaliojitokeza katika mpango wa uanzishwaji shule za kata.

Hata hivyo kabla ya kuishuhudia bajeti hiyo ikiwasilishwa Dk. Mkumbo na Mkenda wakiongozwa na mhadhiri mwenzao kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano, Ayoub Rioba waliwasilisha mada zilizokuwa zikiiangalia elimu ya Tanzania na majaliwa yake.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Elimu tayari imewasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2012/13 ambapo jumla ya sh. 724,471,937,000 ili zitumike kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake. Huku sh. 18,561,689,000 zikiwa ni fedha za ndani na sh. 74,019,627,000 kutoka kwa washirika wa maendeleo.