Somalia
WATU zaidi ya 750,000 huenda wakafa njaa kutokana na makali ya ukame katika miezi ijayo, hii ni onyo iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ikitangaza njaa katika eneo jingine jipya.
Umoja wa Mataifa unasema maelfu ya watu wamekufa baada ya kile kinachotajwa kuwa ukame mbaya zaidi kuikumba Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka 60. Eneo la Bay limetajwa kama eneo la sita kutangazwa rasmi kuwa na njaa katika sehemu za kusini mwa Somalia zinazotawaliwa na wapiganaji wa al Shabab. Umoja wa Mataifa unasema watu milioni 12 katika eneo hilo wanahitaji msaada wa chakula.
Kwa jumla watu milioni 4 wanakabiliwa na matatizo ya chakula Somalia ambapo watu 750,000 wako katika hatari ya kufa katika miezi minne ijayo kutokana na ukosefu wa msaada unaohitajika kwa dharura. Tamko la idara ya chakula na ufafanuzi wa lishe bora-FSNAU. Idadi ya watu wanaokufa katika eneo la Bay sasa imefika idadi ambayo inaliorodhesha eneo hilo kutangazwa rasmi kuwa linakabiliwa na njaa.
Nchi jirani za Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya na Uganda pia zinatatizika kutokana na ukosefu wa mvua. Mwandishi wa BBC katika eneo la Afrika Mashariki Will Ross anasema kuwa ni vigumu sana kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu kuwafikia watu katika maeneo yanayokaliwa na wapiganaji wa al Shabab. Kundi hilo la al Shabab linalohusishwa na Al Qaeda linadhibiti eneo kubwa la kusini mwa Somalia ikiwa ndio sehemu iliyokabiliwa vibaya na ukame nchini humo.
Baadhi ya maafisa wa al Shabab wameyashutumu mashirka ya misaada kutoka mataifa ya magharibi kuwa yanaongeza chumvi kuhusu hali halisi ya mambo kwa malengo yao ya kisiasa. Mwandishi wa BBC anasema kiasi cha msaada wa chakula kinafika katika sehemu hiyo lakini sio kwa kiwango kinachohitajika.