Wasimamizi wa BVR Dar es Salaam Wanolewa Kimaandalizi

Wasimamizi wa uandikishaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura katika jiji la Dar es salaam wakiwa katika mafunzo hayo.

Wasimamizi wa uandikishaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura katika jiji la Dar es salaam wakiwa katika mafunzo hayo.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Raymond Mushi akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kufungua mafunzo ya wasimamizi wa uandikishaji wa Wananchi katika Daftari la Kudumu la wapiga kura kupitia mfumo wa BVR litakalofanyika Julai 16 hadi 25 mwaka huu.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Raymond Mushi akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kufungua mafunzo ya wasimamizi wa uandikishaji wa Wananchi katika Daftari la Kudumu la wapiga kura kupitia mfumo wa BVR litakalofanyika Julai 16 hadi 25 mwaka huu.

Na Aron Msigwa – Dar es Salaam

SERIKALI imesema kuwa zoezi la uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR jijini Dar es salaam litafanyika kama ilivyopangwa kuanzia Julai 16 hadi 25 mwezi huu kwa mafanikio makubwa kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanywa na Tume ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Manispaa za mkoa huo.

Akizungumza wakati ufunguzi wa Mafunzo ya siku 2 ya wasimamizi wa uchaguzi wa mkoa huo leo jijini Dar es salaam, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw. Raymond Mushi alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wasimamizi wa Manispaa hizo ili zoezi la uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura katika jiji la Dar es salaam lifanyike kwa kiwango cha hali ya juu na kuzuia makosa yaliyojitokeza katika maeneo
mengine nchini.

Amewataka wasimamizi hao kufanya kazi kwa viwango na weledi wa hali ya juu ili kuzuia malalamiko kutoka kwa wananchi kwa kuhakikisha kuwa kila raia mwenye sifa anaandikishwa katika daftari hilo.

Alisema kuwa wananchi wote watakaofika kwenye vituo kujiandikisha wahakikishe kuwa wana taarifa muhimu kuhusu uraia wao pia wahakikishe kuwa wanafuata taratibu zilizowekwa na Tume ili waweze kuandikishwa.

“Natoa wito kwa wananchi wote waliokidhi viwango vya kupiga kura na wale watakaofikisha umri wa kupiga kura ifikapo 25 Oktoba 2015 wajitokeze kwa wingi maana wote wataandikishwa,” alisisitiza.

Aidha, amewataka wasimamizi hao kufanya kazi kwa weledi, kutoa ufafanuzi na elimu kwa wananchi pale inapobidi wakati wa ukusanyaji wa taarifa zao na kuepuka kutumia lugha ya kuudhi ili kazi hiyo iwe rahisi na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika kujiandikrsha na kuepuka vitendo vya vurugu na siasa zinazoweza kuleta machafuko katika vituo vya uandikishaji.

Ametoa wito kwa baadhi ya wanasiasa watakaofika kujiandikisha kwenye daftari la kudumu kuepuka kuingilia zoezi hilo kwa kuwa wao sio watumishi wa Tume ya uchaguzi.

“Kuna maeneo nchini baadhi ya wanasiasa wamekuwa chanzo cha kusababisha vurugu kwenye vituo vya uandikishaji, wao kama raia wanalo jukumu la kufika kujiandikisha na kuangalia watu wanaojiandikisha kama sehemu ya haki na wajibu wao kufuatilia ufanisi wa zoezi hilo na sio
kuingilia kazi za wataalam wa Tume”.

Kwa upande wake Ofisa TEHAMA Mwandamizi kutoka Tume ya Uchaguzi Bw. Joseph Mally, Ofisa Amesema kuwa Mafunzo hayo ya siku 2 yaliyohusisha wasimaizi 36 wa uchaguzi ngazi ya jimbo kwa manispaa zote tatu Ilala, Kinondoni na Temeke ambao nao watatoa mafunzo hayo kwa wasimamizi wa Kata 36, ujazaji wa Fomu na matumizi ya mashine za BVR. Alisema wao kama Tume ya Uchaguzi watahakikisha kuwa wanatembelea vituo vyote vya uandikishaji ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza.

Aidha kwa kuzingatia wingi wa idadi ya watu katika jiji la Dar es salaam kutakuwa na mashine 3500 zitakazofanya kazi katika vituo 1000 huku kukiwa na wataalam zaidi ya 600 waliopatiwa mafunzo kwa lengo la kukamilisha kazi hiyo na kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika maeneo mengine.

“Kwa upande wa Tume tunaendelea kujipanga ili kuhakikisha kuwa changamoto zilizotokea katika maeneo mengine hazitokei, tunatoa wito kwa wananchi watakaofika kwenye vituo kuandikishwa wawe wamekidhi vigezo vilivyowekwa kulingana na vielelezo vya uraia, na umri,” Amesema.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo kutoka Manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mafunzo hayo wamesema kuwa mafunzo hayo ya siku 2 yanawajengea uwezo wa kuelewa namna ya kuandikisha wapiga kura, ujazaji wa fomu, uelewa wa sifa za mtu anayestahili kuandikishwa na matumizi ya mashine za BVR.