RIPOTI ya viashiria vya Ukimwi nchini katika mwaka 2011/12 imeonyesha kuwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 23 na 24 wameambukizwa virusi vya Ukimwi kwa asilimia 6.6, ikilinganishwa na wavulana wa umri huo ambao ni asilimia 2.8. Akisoma ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania, (Tacaids), Dk Fatuma Mrisho alisema kiwango cha wasichana wa umri huo wenye virusi ni mara mbili zaidi ya wavulana.
Akizindua ripoti hiyo, Rais Jakaya Kikwete alisisitiza Watanzania na sekta zote zinazojihusisha na mapambano dhidi ya Ukimwi, zitilie mkazo umuhimu wa kukomesha unyanyapaa na kuhamasisha upimaji wa hiari.
“Watanzania zaidi ya milioni mbili wamefariki tangu Ukimwi ugundulike miaka 30 iliyopita, tunatakiwa tupambane kwa dhati kabisa,” alisema Rais Kikwete.
Alipongeza ongezeko la idadi ya watu waliopima kwa hiari na kuwataka wanaume kupima badala ya kuwaachia jukumu hilo wanawake.
Rais pia alizitaka taasisi za Ukimwi, kudhibiti kasi ya maambukizi katika miji mikubwa na katika barabara kuu zikiwemo za Chalinze na Njombe.
“Maeneo hayo yanahitaji nguvu zaidi, hata maeneo yenye kiwango kidogo cha maambukizi nayo yasibweteke yanahitaji tahadhari,” alisema.
Kuhusu tohara kwa wanaume, Rais Kikwete alisisitiza zaidi tohara kwa wanaume na kwamba wasiotahiriwa wanaongeza kasi ya maambukizi kwa asilimia 60 na wanaotahiriwa wanapunguza kwa asilimia 60 pia.
Kwa upande wake, Dk Kikwete alisema maambukizi kwa vijana wenye umri mdogo yanatokea wakati vijana hao wana umri wa kati ya miaka 15 na 19 na matokeo yake kuwa wazi katika umri wa miaka 23 na 24. Alisisitiza kuwa matokeo haya ni kama ya sensa na kwamba si kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 14 hadi 49 amepimwa.
“Kwa jumla asilimia 2.0 ya wasichana na wavulana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wana maambukizi ya virusu,” alisema. Hata hivyo ripoti hiyo ilionyesha kuwa kasi ya maambukizi kwa Tanzania nzima, imepungua kutoka asilimia 5.8 mwaka 2008 hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2011/2012.
Utafiti wa kwanza wa aina hii ulifanywa mwaka 2003 -2004 ambapo maambukizi yalikuwa asilimia 7.06. Utafiti mwingine ulifanyika mwaka 2009-2010 ambapo maambukizi yalishuka toka asilimia 7 hadi asilimia 5.8
Pia, ripoti hiyo ilionyesha kuwa asilimia tisa ya wasichana na 10 ya wavulana wenye umri wa miaka 15 na 24 walianza kujamiiana kwa mara ya kwanza kabla ya kutimiza miaka 15.
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa Mkoa wa Njombe una maambukizi ya juu zaidi ya asilimia 14.8 ya maambukizo kuliko mikoa yote Tanzania.
Maeneo ya visiwani yana asilimia ndogo zaidi ya maambukizi ambapo Unguja ilikuwa na asilimia 1.2 na Pemba asilimia 0.5 tu
“Matokeo ya ripoti hii yatatupa mwanya zaidi wa kujua nini kifanyike na wapi nguvu iongezwe katika kupambana na maradhi haya hatari,” alisema Kikwete.
Takwimu za sasa zinaonyesha kuwa maeneo ya mijini yana maambukizi mengi zaidi ambapo kwa wanawake ni asilimia 6.2 na wanaume ni asilimia 3.8, Ripoti hiyo ilionyesha kuwa zaidi ya robo ya Watanzania walioko kwenye ndoa wana maambukizi ya Ukimwi.
CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz