Na Mtuwa Salira, EANA
Wasanii na wanamuziki wametakiwa kutumia vipaji vyao kuchora na kutunga nyimbo zinazohamasisha masuala ya haki za binadamu katika jamii.
”Wanasanaa na wanamuziki wana jukumu kubwa na wana nafasi muhimu ya kuhamasisha uelewa wa wananchi kuhusu haki za binadamu na watu nchini Tanzania na maeneo mengine,” alisema Rais wa Mahaka ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Augustino Ramadhani alipokuwa anapokea michoro nane ya Tinga Tinga inayoonyesha masuala ya haki za binadamu katika makao makuu ya mahakama hiyo jijini Arusha mwishoni mwa wiki.
Jaji Ramadhani alitoa wito huo baada ya kukabidhiwa michoro hiyo na msanii kutoka Dar es Salaam, Lewis Mseza ambaye alilazimika kuchora michoro hayo baada ya mtoto wake hivi karibuni kukumbwa na unyanyasaji wa polisi na kutotendewa haki na mahakama.
”Kazi nzuri ya uchoraji wa msanii Mseza hainabudi kuigwa na wasanii wengine wenye vipaji kama vile wanamuziki nchini na katika bara zima,” alisema Jaji huyo ambayo pia ni Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania katika sherehe ambayo ilihudhiriwa pia na majaji wengine wa mahakama hiyo ambao hivi sasa wako katika kikao chao cha mahakama cha kawaida cha wiki tatu.
Katika harakati za uhamasishaji endelevu wa masuala ya haki, nchi za Afrika zinaweza kuweka utamaduni imara wa demokrasia kwa ajili ya maendeleo ya watu wake.
Kwa upande wake Mseza alisema ataendelea na kazi yake ya kuelimisha watu juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu kupitia michora yake.
”Mimi ni muathirika wa ukiukwaji wa haki zangu za msingi za binadamu na nitaendelea kuhamashisha masuala ya kupigania haki za biadamu kupitia kazi yangu ya sanaa,” alisisitiza.
Sanaa ya michoro ya Tinga Tinga yenye muda wa zaidi ya miaka 40 baada ya kifo cha mwanzilishai wake Saidi Tingatinga ni miongoni mwa michoro yenye mvuto wa aina yake katika sanaa za Afrika.
Kwa bahati mbaya Tingatinga mwenyewe pia alikuwa ni muathirika wa tukio la polisi.Usiku mmoja mwaka 1972 Tingatinga alipigwa risasi na kufa kwa bahati mbaya akidhaniwa kuwa ni mwizi aliyekuwa anawakimbia polisi.