Na Mwandishi Wetu
WASANII mbalimbali nchini wanatarajiwa kutoa burudani katika pambano la mchezo wa ngumi lisilo na ubingwa litakalowakutanisha bondia, Mada Maugo na mpinzani wake Suleimani Saidi ‘Toll’ Desemba 18 mwaka huu katika Ukumbi wa Mzalendo Pub Kijitonyama Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na burudani Rais wa shirikisho la ngumi za kulipwa nchini (PST), Emanuel Mlundwa alisema, maandalizi kwa ajili ya pambano hilo yamekamilika.
Aliwataja wasanii watakaotoa burudani siku hiyo kuwa ni Kundi la mapacha watatu Khalid Chokoraa (Halidi Chuma) pamoja na msanii wa mziki wa bongo fleva Mwana FA (Hamisi Mwinjuma).
Alisema licha ya kuwepo kwa burudani hizo vile vile atakuwepo kocha wa mchezo wa ngumi Rajabu Mhamila Super D kwa ajili ya kutoa mafunzo kupitia Dvd pamoja na kuzisambaza.
Aliwataka mashabiki wao wajitokeze kwa wingi kushuhudia burudani hiyo, licha ya kuwa mchezo huo haupewi kipaombele watahakikisha wanasonga mbele katika kuazimisha miaka 50 ya uhuru.
Aidha katika mapambano ya ngumi ya utangulizi itakuwa ni mabondia Yohana Miyayusho na Shadrack Juma, Doto Kipacha atazidunda na Saidi Muhidini huku kwa upande wa mchezo wa Kick Boxing ambao utatuwakilisha kimataifa Tanzania, Muaythai Academy of Combat wameandaa pambano kwa mara ya kwanza nchini kati ya bondia Emanuel Shija kutoka Tanzania na Munyeshyaka Vincent kutoka Rwanda. Mpambano huo utakuwa wa kimataifa kutokana na ushiriki wake wa nchi hizo mbili ambazo zitakuwa na bendera zao.
Chanzo; Super D Boxing Coach