Wasanii Bongo na thamani ya Big G

Hamad Ally a.k.a Madee ‘Rais wa Manzese’

TANGU kuanza kwa muziki wa kizazi kipya hapa Bongo, mamia ya vijana wamejitokeza kuonyesha vipaji vyao katika fani hiyo na kufanya kuwepo kwa familia kubwa ya wasanii wanaotamba katika muziki huo uliobatizwa jina la Bongo Flava.

Uwepo wa muziki wa Bongo flava, umekuwa na faida kubwa kwa vijana wa taifa hili na kuufanya muziki huo kuchukuliwa kama mkombozi kwa kugeuka ajira kwa vijana, hasa kwenye wakati huu wa maisha magumu na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wengi katika taifa hili linalosifika kwa amani na upendo duniani kote.

Lakini licha ya vijana hao kujitokeza kwa wingi na kukubalika kwa kazi zao katika jamii ya wapenda burudani nchini, kuna jambo la ajabu ambalo limekuwa likiwaacha watu vinywa wazi juu ya uwezo wa kweli wa wasanii husika wa kimuziki huo.

Hii inatokana wasanii hao, ambao wengi wao wamekuwa wakiibuka kwa kasi na kujipatia umaarufu wa haraka lakini wamekuwa wakipotea kama upepo uvumao kwa kasi, bila ya sababu zinazoeleweka na kuwawafanya kutoonekana juu ya majukwaa ya kizazi kipya.

Katika zama za mwanzo za muziki huu, wapo wasanii ambao kwa kiasi kikubwa walitamba na kutisha kwa kiasi kikubwa katika Bongo Flava, walichokifanya katika muziki huo kilifanikiwa na waliweka nguvu kubwa katika kuukuza muziki huu, lakini leo hii ni nadra sana kuwasikia, nini kimewapoteza?.

Kila shabiki wa muziki huo anafahamua uwezo na ukali wa kuimba aliokuwanao nyota wa muziki huo Aboubakar Shaaban Katwila ‘Q-chilla’ wakati anatoka kwa mara ya kwanza na wimbo wake wa ‘Aseme’.

Hakika kijana huyu alikuwa kivutio na tishio kubwa kwa wasanii wengine kiasi kwamba wengi wao walikuwa wakitamani kufanya naye ‘kolabo’ tu ili kujiongezea nguvu katika ‘gemu’.

Lakini leo hii, Q –Chilla amekuwa kimya sana kiasi kwamba baadhi ya mashabiki wanadiriki kusema kuwa ‘amefulia’ na wengine wakidai kwamba huenda ndiyo kapotea katika game wakati bado wadau wanahitaji huduma ya sauti yake na ujumbe katika nyimbo zake.

Siyo Q-Chilla peke yake, msanii Philipo Nyandindi ‘O-ten’ ambaye alitamba sana na wimbo wa ‘Nicheki’ ambao kwa kiasi kikubwa ulimpa mafanikio ikiwemo ya kununua gari zuri la kisasa, leo hii hajulikana alipo na bado haijulikani tatizo ni nini?

Huu ni mfano tu wa wasanii wengi ambao thamani yao kwenye muziki imekuwa kama ‘Big G’, ambayo inakuwa na utamu pale unapoanza kuitafuna lakini baada ya muda hutopenda kuendelea kuiweka mdomoni.

Haifahamiki tatizo ni nini, labda ni aina ya muziki wanaoimba kutokuwa na nguvu sana ya kuendelea kuwaweka juu? ama ni uchache wa uwezo wao katika kutunga na kuimba nyimbo zinazoweza kuwafanya wakae katika fani kwa muda mrefu.

Au ni kupigwa kwa nyimbo zao mara kwa mara katika vyombo vya habari na kuzifanya ziondoke katika chati kwa haraka? Kama siyo hivyo basi labda ni kulewa sifa za haraka kwa wasanii hao ndiko kunakowaporomosha.

Lakini pia, kuna wasiwasi mkubwa juu ya elimu ya kutosha ya muziki wana Bongo flava hawa, hilo ndiyo jambo linalowafanya wasanii hao kushindwa kutambua njia sahihi za kuwafanya kubaki juu kimuziki, hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao wameibukia mtaani tu bila kupitia shule, ama vyuo vya muziki.

Hamis Mwijuma a.k.a Mwana FA.

Unaweza kujiuliza jambo hili pale utakapoichunguza safari ya muziki inayomuhusu Gwiji la muziki la Afrika, Koffi Charles Antoine Olomide ‘Kuadra Kora man’ ambaye tangu alipotoka mara ya kwanza, hajawahi kushuka kimuziki hata kidogo, licha ya kuwa amekuwa akiondokewa na waimbaji nyota anaowalea na kuwafundisha mwenyewe katika bendi yake ya QR International.

Koffie mbali na kusomea muziki lakini ana elimu ya uchumi ambayo kwa njia moja ama nyingine inamsadia katika kujipangia mambo ya kufanya katika muziki wake.

Mashabiki wengi wa Bongo flava, wanalia na aina ya muziki ambao wasanii wao wanaoupiga na kuonekana ni wakuiga zaidi badala ya kuwa ule unaotokana na kuumiza vichwa vyao.

Katika hili kuna aina nyingi za muziki ambao wasanii hawa wangeweza kuzitumia ili kuongeza ubunifu wao, mfano wangeweza kutafuta mtindo kutoka tamaduni za Kitanzania, jambo ambalo pengine lingewafanya kukaa juu kitaifa na kimataifa kutokana na ubunifu wao huo.

Wangeweza kufanya utafiti wa muziki wa Tanzania na kutoka kivyao tofauti na staili zao muziki wao wa sasa, Mtu anaweza kukaa Bongo kwa miaka kadhaa lakini asijue wasanii hao wanatumia mtindo gani, lakini kamwe huwezi kuchukua hata dakika mbili kuujua muziki kutoka Jamuhuri ya Congo (DRC) unatumia mtindo gani, kama ilivyo pia kwa muziki kutoka, Afrika Kusini Jamaica na India.

Huenda hili likawa jibu la moja kwa moja juu ya kile kinachowakuta wasanii wetu na kufanya kazi za Big G, ni wazi kuwa mashabiki bado wana kiu kubwa ya kusikia kazi za kweli kutoka kwa akina Ferouz, Daz Baba, O-ten, Pig Black, King Crazy GK, Snare, Caz T, wengine wengi waliokuwa wakitamba hapo awali katika kuusongesha muziki wa Tanzania.

Mpaka leo hii kiu kubwa ya wapenzi wa muziki wa Tanzania inabaki kukatwa na akina Mbaraka Mwinshehe, Marijani Rajabu,Juma Ubao na wengine ambao walikuwa wakimpa wakati mgumu marehemu Rwambo Luanzo Makiadi ‘Franco’ kila alipokuwa akija nchini licha ya kuwa alikuwa amejijengea umaarufu duniani kote.

Jamani lengo la makala haya si kurushiana lugha chafu, bali ni kutafuta kupiga hatua tu katika kile ambacho tunahisi kuwa hiki ni cha nyumbani kwetu hivyo tusaidiane kwa hilo wadau.

Ni Mtazamo tu.
source www.globalpublishers.info