RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa baadhi ya wahamiaji haramu wanaoishi katika Mkoa wa Kagera, hususan katika Wilaya ya Kagera, siyo wavamiaji bali wanakaribishwa na kupewa vibali haramu vya kuishi nchini na maofisa wa Serikali.
Aidha, Rais Kikwete amewataka wageni hao haramu kujiondoa wenyewe nchini na kurejea makwao katika wiki mbili zijazo kwa sababu Tanzania haitaki ugomvi na majirani hasa Serikali itakapowasaka na kuwafukuza nchini.
Akizungumza kabla ya kuzindua mradi wa kusambaza umeme katika vijiji 16 vya Wilaya ya Karagwe kwenye Kijiji cha Nyakayanja, Nyaishozi, Wilayani Karagwe Jumamosi, Julai 27, 2013, Rais Kikwete amewaambia wananchi ambao walikuwa wamelalamikia kero ya wahamiaji haramu katika Wilaya hiyo, Rais amesema:
“Wengine hawa hawavamii, siyo wavamizi wa kweli bali mnawakaribisha nyie kwa sababu ukiwauliza hawa watakuonyesha vibali vya kuishi nchini ambavyo vimetolewa na maofisa watendaji ama wa vijiji ama wa watendaji wa kata, ama watendaji wa tarafa ama madiwani.”
“ Maofisa hawa wa Serikali wanajifanya maofisa uhamiaji. Lakini haina taabu kwa sababu tutawasaka wahamiaji haramu wote katika wiki mbili zijazo, tutawakamata na kuwarudisha makwao. Hili la wahamiaji haramu haliwezi kumalizika kwa sababu vibali vya kuishi vinatolewa na maofisa wetu wa Serikali. Hali hii haiishi kama watoa vibali bado wapo. Ni lazima tuwakomeshe hawa.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Na ni vizuri wakajiondoa na kurudi kwao mapema. Hili litakuwa jambo zuri kwa sababu sisi hatutaki ugomvi na majirani zetu. Tunataka kuishi kwa amani na upendo. Hatutaki wahamiaji hawa haramu watugombanishe na majirani wetu. Warudi kwao mapema.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Baya zaidi ni kwamba kinatolewa kibali kimoja, lakini hicho hicho kinaingiza watu chungu nzima kwa kufanyiwa photocopy (nakala kivuli). Kila mtu anaingia kwa hicho. Mwenye kibali cha kuingiza ng’ombe ishirini anaingiza 200.”
Amefafanua Rais: “Ni kweli wapo wavamizi katika lile Pori la Burigi. Nasikia wengine juzi wamekurupushwa wakakimbia na ng’ombe wao lakini wakasahau ndama mmoja. Pori la Burigi siyo ranchi ni hifadhi ya taifa. Tutawatoa hawa.”
“Hawa walioko vijijini kwetu tutajua nani kamkaribisha nani. Wahamiaji haramu tutawasaka na kuwafukuza na wale watumishi wa Serikali waliowakaribisha na kuwapa vibali vya kuishi tutawachukulia hatua.”
Kauli hiyo ya Rais kuhusu wahamiaji haramu inafuatia amri yake aliyoitoa jana, Ijumaa, Julai 26, 2013, akiwa mjini Biharamulo ambako alitoa wiki mbili kwa majambazi wanaoteka magari na kuua watu na wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita kujisalimisha wenyewe pamoja na silaha zao kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Baada ya wiki mbili, Rais Kikwete, amevielekeza vyombo vyote vya ulinzi na usalama – Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Idara ya Uhamiaji – kuanzisha operesheni kubwa kuliko zote zilizowahi kufanyika nchini kuwasaka kila mahali na kuwatia mbaroni majambazi na wahamiaji hao haramu.
Na Rais Kikwete ameonya: “Na wala operesheni hii haitakuwa ya muda mfupi, siyo homa ya vipindi hii. Operesheni hii haitaisha mpaka tatizo lenyewe liishe. Na lazima wananchi wasaidie katika kumaliza tatizo hili kwa sababu ulinzi na usalama ni jukumu la kila Mtanzania, na hasa kila mzalendo, yaani kila mmoja wetu.”
Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku sita katika Mkoa wa Kagera na Julai 28, 2013, atatembelea Missenyi.
WAKATI HUO HUO, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Julai 27, 2013, amezindua rasmi Kivuko cha Mv. Ruvuvu kitakachofanya kazi kwenye Mto Ruvuvu katika eneo la Rusumo, Wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera.
Aidha, Rais Kikwete amezindua Mradi Mkubwa wa Kusambazwa Umeme katika vijiji 12 vya Wilaya ya Karagwe katika sherehe iliyofanyika katika Kijiji cha Nyakayanja, Nyaishozi wakati akiwa njiani kutoka Wilaya ya Ngara kwenda Wilaya mpya ya Kyerwa..
Rais Kikwete amezindua miradi hiyo miwili na kivuko kipya na mradi wa umeme ikiwa ni moja ya shughuli zake za kukagua miradi ya maendeleo katika ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Kagera. Miradi hiyo yote imegharimiwa na Serikali ya Tanzania.
Kivuko cha Mv Ruvuvu kinachukua nafasi ya kivuko cha zamani ambacho kimezeeka na kilikuwa kimeanza kuonekana hatari kwa wasafiri waliokuwa wanatumia kivuko hicho na uzinduzi huo wa kivuko kipya ni utekelezaji wa ahadi ya uchaguzi mkuu wa Chama cha Mapinduzi ambacho Mheshimiwa Kikwete ni Mwenyekiti wake.
Kivuko hicho kilichonunuliwa kwa thamani ya Sh. bilioni 2.9 kilijengwa nchini Uholanzi, kina uwezo wa kubeba abiria 50 waliokaa, abiria 30 waliosimama na magari matano wadogo.
Akizungumza kabla ya kumwalika Rais Kikwete kuzindua kivuko hicho, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli amesema kuwa kuzinduliwa kwa kivuko hicho ni mwanzo wa uzinduzi wa vivuko 25 ambavyo tayari ujenzi wake umekamilika ama unakamilika ama karibu kuanza na ambavyo gharama zake zote zinalipwa na Serikali ya Tanzania.
Baadhi ya vivuko hivyo ni Mv. Ujenzi (Ukerewe), Mv. Musoma (eneo la Kinesi Mkoani Mara), Mv. Karambo, Mv. Msanga Mkuu, Mv. Ilagara, Mv. Kaunda na kivuko kikubwa kitakachofanya safari zake kati ya Dar Es Salaam na Bagamoyo kwa nia ya kupunguza msongamano katika Jiji la Dar Es Salaam. Kivuko hicho cha Dar Es Salaam-Bagamoyo kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 300 kwa wakati mmoja na kitajengwa kwa gharama ya Sh. bilioni tisa.
Magufuli pia amewaambia wananchi kuwa wanafunzi wenye sare za shule watatumia kivuko hicho cha Mv. Ruvuvu bila malipo yoyote kama ilivyo sera ya Serikali kwa vivuko vyote nchini kwa wanafunzi.
Mara baada ya kumaliza sherehe za kuzindua kivuko hicho, Rais Kikwete amesimama kwa muda kukagua ujenzi wa Kituo Kimoja cha kuhudumia shughuli za mpakani kati ya Tanzania na Rwanda eneo la mpakani Rusumo badala ya kila nchi kuwa na kituo chake na hivyo kuchelewesha usafirishaji wa mizigo na usafiri wa abiria kati ya nchi hizo mbili.
Rais Kikwete ameambiwa kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Kituo hicho, yatakuwepo majengo mawili tofauti, moja kwa kila nchi, lakini Kituo cha kurahisisha usafirishaji na usafiri kitakuwa kimoja tu.
Ameambiwa kuwa Kituo hicho kitafanya kazi kwa saa 24 kwa siku na kitaweza kupitisha idadi kubwa ya magari kati ya 400 na 500.
Kuhusu Mradi wa Umeme, Rais Kikwete ameambiwa kuwa uzinduzi uliofanywa leo utanuisha vijiji 12 ambako zitajengwa njia za umeme zenye urefu wa kilomita 25 za msongo wa kilowati 33. Tayari wateja 345 wameunganishiwa umeme kutokana na mradi huo.
Awamu hiyo ya usambazaji umeme katika Wilaya ya Karagwe ni sehemu ya kusambaza umeme katika Wilaya hiyo na Wilaya ya Bukoba Vijiji ambao unagharimu Sh. bilioni 16.
Rais Kikwete pia ameambiwa kuwa itakuwepo awamu ya pili ya usambazaji umeme katika Mkoa wa Kagera ikiwamo Wilaya ya Karagwe ambako vijiji vingine 30 vitaunganishwa kwenye umeme kwa gharama ya Sh.bilioni 60. Awamu hiyo ya pili inatarajiwa kuwanufaisha wateja 26,000.
Akizungumza kwenye sherehe za uzinduzi wa mradi huo, Rais Kikwete amesema kuwa hakuna maendeleo bila umeme. “Huwezi kuendesha mitambo kwa koroboi ama chemli.”