RAIS Mohamed Mursi leo Desemba 08, 2012 alitarajiwa kufanya mazungumzo juu ya kumaliza mzozo mbaya nchini Misri tangu achukue madaraka. Hata hivyo viongozi wakuu wa upinzani nchini humo wameapa kuwa hawatashiriki mazungumzo hayo. Cairo pamoja na miji mingine imekumbwa na maandamano ya vurugu tangu Novemba 22, wakati Mursi alipotangaza amri akijipa madaraka makubwa zaidi ambayo yanamuweka juu ya sheria.
Mvutano huo katika taifa hilo la Kiarabu lenye wakaazi wengi zaidi, kufuatia kuanguka kwa utawala wa rais wa zamani Hosni Mubarak mwaka jana, kunaleta hofu katika mataifa ya magharibi, hususan Marekani, ambayo imeipatia nchi hiyo fedha nyingi kwa ajili ya jeshi la nchi hiyo na misaada mingine tangu pale Misri ilipotia saini ya makubaliano ya amani na Israel mwaka 1979.
Huenda upigaji kura ukasitishwa
Naibu wa Mursi ameonyesha uwezekano kuwa kura ya maoni ambayo imepangwa kufanyika hapo Desemba 15 kwa ajili ya katiba mpya ambayo inapingwa na watu wenye msimamo wa wastani huenda ikacheleweshwa. Hata hivyo imeelezwa kuwa tume ya uchaguzi nchini Misri imeahirisha upigaji kura kwa watu wanaoishi nje ya Misri, lakini kura hiyo itafanyika hapo Desemba 15 kama ilivyopangwa.
Maridhio hayo hata hivyo yanakwenda tu umbali wa kukubali madai yanayotolewa na upande wa upinzani, ambao pia wanataka Mursi kuondoa kabisa amri ambayo inampa madaraka makubwa.
Ikulu yavamiwa
Siku ya Ijumaa ya Desemba 07, 2012 kundi kubwa la waandamanaji lilivamia eneo la kuzunguka Ikulu ya rais, wakivunja vizuizi vya waya na kupanda juu ya vifaru vya jeshi vinavyolinda jengo hilo la rais wa Misri aliyechaguliwa kwa njia huru na haki, na ambaye aliingia madarakani mwezi Juni. Wakati usiku ukitanda, mamia kwa maelfu ya wafuasia wa upinzani bado walikuwa katika eneo la ikulu hiyo, wakipunga bendera na kumtaka Mursi, kuondoa.
“Tutakaa hapa kwa muda wowote na tutaendelea kutayarisha maandamano kwingineko hadi pale rais Mursi atakapofuta tamko lake la amri ya kikatiba na kuahirisha kura ya maoni,” amesema Ahmed Essam, mwenye umri wa miaka 28, mhandisi wa kompyuta na mwanachama wa chama cha kiliberali cha Dostour.
Makamu wa rais Mahmoud Mekky alitoa taarifa akisema kuwa rais yuko tayari kuahirisha upigaji kura ya maoni iwapo hiyo itafanyika bila ya kupingwa kisheria. Mkutano wa majadiliano yaliyopangwa na Mursi unatarajiwa kufanyika leo Jumamosi (08.12.2012) bila ya kuwapo makundi kadha ya upinzani.
Mursi kuendelea na majadiliano
Mursi anaweza kuungana na viongozi wakuu wa mahakama pamoja na wanasiasa kama Ayman Nour, mmoja wa wagombea katika uchaguzi pekee uliohusisha wagombea wengi wakati wa utawala wa rais Mubarak , mwaka 2005, ambapo alishindwa vibaya.
Upinzani unadai kuwa Mursi aondoe tamko lake la amri linalompa madaraka makubwa na kuchelewesha kura ya maoni iliyopangwa kufanyika hapo Desemba 15 kuhusu muswada wa katiba ya nchi hiyo iliyoundwa na baraza lililoongozwa na vyama vya Kiislamu, ambayo wanadai ina mapungufu na inakosa kufikia matakwa ya Wamisri wote.
-DW