Na Mwandishi Wetu
RAIA wanne wa mataifa tofauti, jana wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, kwa kosa la kula njama na kuingiza dawa za kulevya nchini zenye thamani ya sh
bilioni 2.8.
washtakiwa hao ambao ni Dennis Okechukwa, Paul Obi ambao ni raia wa Nigeria, mwingine ni
raia wa Afrika Kusini, Stani Hycenth pamoja na raia wa nchini Pakistan ambaye alitajwa kwa
jina la Shoaib Ayaz, wote walisomewa mashtka mawili mahakamani hapo.
Wakili wa upande wa mashitaka, Prosper Mangamila akisaidina na Biswalo Mganga, walisoma
mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mustapher Syani, ambapo ilidaiwa katika shtaka la kwanza
washtakiwa hao wanatuhumiwa kwa kosa la kula njama.
Mwangamila alidai katika siku tofauti kati ya Septemba 26, mwaka jana na Machi 4, mwaka huu
katika maeneo tofauti katika nchi za Tanzania, Nigeria, Afrika Kusini na katika maeneo
tofauti nchini Pakistan washtakiwa hao walikula njama ya kutaka kusafirisha dawa za kulevya
kwa nia ya kuleta nchini.
Alidai katika shtaka la pili ambalo watuhumiwa hao wanatuhumiwa kusafirisha dawa za kulevya,
ilidiwa Machi 4 mwaka huu, huko Kunduchi Mtongani washtakiwa kwa pamoja waliingiza nchini
dawa za kulevya aina ya Heroine gramu 81,000 zenye thamani ya sh 2,835,000,000.
Wakili anayewatetea washtakiwa hao Braison Shayo, aliiomba mahakama kutoa kibali cha
washtakiwa hao kurudishiwa simu zao ili wawasiliane na ndugu zao kwakuwa washtakiwa hao si
raia wa Tanzania.
Hoja hiyo ilipingwa na mawakili wa upande wa mashitaka, ambapo alidai wakili huyo ametumia
kifungu gani cha sheria na kwamba hakuna sheria inayoruhusu vitu vilivyokamatwa kwa ajili ya
uchunguzi kurudishwa kwa mshtakiwa.
Mganga alidai kimsingi mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa au kuruhusu mali hizo kurudishwa
kwa mshtakiwa kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Wakili huyo wa upande wa mashtaka aliendelea kudai kifungu 38 cha sheria ya makosa ya
mwenendo wa jinai (CPA), kinamruhusu Polisi kukusanya vifaa ambavyo wanaona vinafaa katika
uchunguzi na kwamba kurudishwa kwa mawasiliano kwa washtakiwa hao kutaharibu mwenendo wa
ushahidi kwakuwa kesi hiyo bado inafanyiwa uchunguzi zaidi.
Mahakama ilitoa uamuzi wake, ambapo ilisema haina mamlaka ya kutoa uamuzi wowote kwa hayo
maombi wanayotaka na kwamba wanaweza kuyapeleka Mahakama Kuu ambayo ndio yenye mamlaka ya
kusikiliza shauri hilo, kesi hiyo imehairishwa hadi Machi 21, mwaka huu.