Wang’amuzi vipaji Maboresho Stars Wajichimbia Lushoto, Mujuni Kuichezesha AFC Leopards

Boniface Pawasa

Boniface Pawasa

WANG’AMUZI vipaji 28 wanakutana Lushoto mkoani Tanga kwa siku saba katika mpango maalumu wa maboresho ya Taifa Stars ambapo watatoka na orodha ya mwisho ya wachezaji waliopatikana katika mechi za maboresho hayo zilizochezwa nchi nzima. Katika kikao hicho, wang’amuzi hao watapitia majina ya wachezaji walioteuliwa ikiwemo kuwaangalia tena kwenye video kwa vile mechi zote zilirekodiwa. Wachezaji watakaoteuliwa katika mpango huo baadaye wataingia kambini mkoani Mbeya.
 
Wang’amuzi vipaji ambao wanaoondoka Machi 9 mwaka huu kwenda Lushoto ni Abdul Mingange, Boniface Pawasa, Charles Mkwassa, Dan Korosso, Dk. Mshindo Msolla, Edward Hiza, Elly Mzozo, Hafidh Badru, Hamimu Mawazo, John Simkoko, Jonas Tiboroha, Juma Mgunda na Juma Mwambusi.
 
Kanali mstaafu Idd Kipingu, Kenny Mwaisabula, Madaraka Bendera, Madaraka Selemani, Mbarouk Nyenga, Mohamed Ally, Mussa Kissoky, Nicholas Mihayo, Peter Mhina, Salum Mayanga, Salvatory Edward, Sebastian Nkoma, Sekilojo Chambua, Selemani Jabir na Shabani Ramadhan.
 
Wengine ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Kidao Wilfred, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana, Ayoub Nyenzi, Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi na Mshauri wa Rais (Ufundi), Pelegrinius Rutayuga.
 
MUJUNI KUICHEZESHA AFC LEOPARDS CC
Mwamuzi Israel Mujuni ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu (CAF) kuchezesha mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho (CC) Afrika kati ya wenyeji AFC Leopards ys Kenya na SuperSport United ya Afrika Kusini.
 
Mujuni katika mechi hiyo itakayochezwa kesho (Machi 8 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya atasaidiwa na Samuel Mpenzu, Josepht Bulali wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Ramadhan Ibada. Kamishna wa mechi hiyo ni Amir Hassan kutoka Mogadishu, Somalia. SuperSport United ilishinda mechi ya kwanza iliyochezwa wiki mbili zilizopita mabao 2-0.