Wandishi wa Al Jazeera Wafungwa Miaka 7, Rais wa Misri Apinga…!

Mmoja wa waandishi wa Al Jazeera, Peter Greste aliyehukumiwa kifungo.

Mmoja wa waandishi wa Al Jazeera, Peter Greste aliyehukumiwa kifungo.

MAHAKAMA nchini Misri imewahukumu kwenda jela kwa kifungo cha kati ya miaka saba na kumi wandishi watatu wa habari wa Shirika la Habari la Al Jazeera waliokuwa wamezuiliwa kwa miezi sita nchini humo.

Taarifa zinasema waandishi hao walipatikana na hatia ya kueneza habari za kupotosha na kushirikiana na kundi la wapiganaji wa Kiisilamu la Muslim Brotherhood. Mmoja wa wandishi hao, Peter Greste, raia wa Australia alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela, huku mwenzake, Baher Mohamed akihukumiwa kwenda jela miaka 10.

Watuhumiwa wengine 11 waliohukumiwa bila ya wao kuwepo gerezani, walipokea vifungo vya miaka 10 kila mmoja. Hukumu ilipotolewa, Greste kwa hasira aligonga mkono wake katika eneo ambako walikuwa wamezuiliwa huku mwenzake akiburuzwa kutolewa mahakamani na walinzi wa gerezani.

Familia za watuhumiwa nao wakaangua kilio. Kesi hii imezua mjadala kwa kulaaniwa kote duniani hasa na mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na mashirika ya habari ya kimataifa. Lakini nchini Misri, vyombo vya habari vilipeperusha habari hiyo kwa utofauti mkubwa.

Al Jazeera – ni shirika linaloonekana kuunga mkono vuguvugu haramu la Muslim Brotherhood na kwa mtanzamo huo, ni adui ya serikali. Peter Greste, ndiye alikuwa anaripoti matukio nchini Misri Disemba mwaka 2013 wakati wa harakati za mapinduzi. Kisha yeye na wenzake wawili wakatuhumiwa kwa kusaidia vuguvugu la kigaidi na kutangaza taarifa za kupotosha dhidi ya serikali na maslahi ya taifa hilo. Madai ambayo serikali ya Australia imekuwa ikikanusha vikali.

Serikali ya Australia ilitoa taarifa yake ikisema kuwa imeshtushwa na uamuzi wa mahakama katika kesi ya Peter Greste. Imeelezea kushangazwa na hukumu iliyotolewa. Serikali imesema haielewi kabisa matukio haya. Shirika la Al Jazeera lenyewe limepinga hukumu iliyotolewa dhidi ya wandishi hao, Peter Greste, Mohamed Fahmy na Baher Mohamed likisema kuwa inakiuka sheria.

Wakati huo huo; Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amesema anajutia uamuzi wa mahakama kuwafunga jela wandishi wa tatu wa shirika la habari la Al Jazeera. Al Sisi alisema kuwa waandishi hao watatu walipaswa kuamrishwa kurejea makwao badala ya kuhukumiwa kifungo jela. Akizungumza kwenye mkutano na wandishi habari rais Al-sisi alisema kuwa kuhukumiwa kwa waandishi hao kumeonyesha picha mbaya kuhusu Misri.
-BBC