Wanawake wawili wachinjwa Magu


IGP, Said Mwema

Na Mwandishi Wetu, Magu

WANAWAKE wawili wameuawa kikataili kwa kuchunjwa katika matukio mawili tofauti wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, Kwa kile kinachodaiwa ni imani za kishirikina.

Jeshi la Polisi wilayani Magu, limethibitisha katika taarifa zake kutokea kwa matukio yote mawili, na kueleza yametokea katika vijiji vya Mwakiloba na Lutubiga, Kata ya Lutubiga wilayani humo, usiku wa kuamkia juzi.

Taarifa zimeeleza kuwa usiku wa kuamkia juzi, watu wasiofahamika walivamia nyumbani kwa Kabula Maduka (50), mkazi wa kijiji cha Lutubiga, ambapo walimkuta akila chakula cha usiku na ndipo wakamshambulia kwa mapanga na kisha kumchinja na kutokomea kusikojulikana.

Mashuhuda wa tukio hilo akiwemo Maduka Maduka, walisema kuwa mwanamke huyo alikuwa akiishi peke yake katika mji huo. Aidha, imeleezwa kuwa usiku huo huo, majira ya saa 7:00, kijiji cha Mwakiloba Kata ya Lutubiga, bibi kizee mmoja, Ng’walu Nhandi (76), mkazi wa kijiji hicho aliuawa kwa kuchinjwa nakitu chenye ncha kali na watu wasiofahamika.

Diwani wa kata hiyo, Kija Gomolo, alisema kuwa bibi kizee huyo alikuwa amelala na wajukuu wake wawili, na kwamba watu hao walipofika walibomoa mlango wa nyumba yake na kumshambulia huku wengine wakizuia ndugu zake waliokuwa wamelala katika nyumba nyingine wasitoke nje.

Diwani Gomolo, alisema kuwa watu hao walimchinja bibi kizee huyo na baada ya kuhakikisha amepoteza maisha walitokomea kusiko julikana. Alisema juzi asubuhi polisi wakiwa na madaktari walifika katika maeneo ya matukio na kuzifanyia uchunguzi miili ya marehemu wote wawili.

“Polisi walifika jana (juzi) asubuhi na kufanya uchunguzi wao na kisha wakaondoka…nakwambia katika kata yetu tumepata matukio haya ya kushitusha sana na kushangaza sana,” alisema.

Polisi walisema kuwa matukio yote mawili yanahusishwa na imani za kishirikina, kwa sababu watu hao baada ya kufanya mauwaji, hawakuchukuwa kitu chochote na kwamba hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa.