Wanawake Watakiwa Kuishi Maisha ya Upendo

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete

Na Anna Nkinda – Maelezo

WANAWAKE nchini wametakiwa kuishi maisha ya upendo, umoja na mshikamano bila ya kuangalia itikadi zao za dini na vyama vya siasa hatua itakayosaidia kuimarisha hali ya amani na  utulivu. Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa futari ya pamoja aliyoiandaa kwa ajili ya wanawake viongozi na wake wa viongozi Ikulu jijini Dar es Salaam .
Mama Kikwete alisema hakuna dini hata moja inayowafundisha watu kuishi maisha ya chuki bali dini zote zinasisitiza kuishi kwa amani, umoja, na upendo jambo ambalo litamfanya binadamu aweze kumfikia  Mwenyezi Mungu.

“Bila ya kuangalia itikadi zetu tulizonazo,  sisi kama viongozi na wake wa viongozi tutumie nafasi tuliyonayo kuzungumza kwa vitendo  maneno matatu ya  upendo, amani na mshikamo ili jamii yetu iweze kuiga mfano kutoka kwetu”, alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wake aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Dk. Asha Rose Migiro alimshukuru Mama Kikwete kwa ajili ya futari aliyoiandaa kwa ajili yao ambayo imewafanya waweze kukutana kwa pamoja na kuweza kubadilishana mawazo.

Dk. Migiro alisema kuwa hivi sasa watu wote wanatakiwa kuliombea taifa amani na salama pia Mwenyezi Mungu awajalie viongozi wote busara, afya njema na mshikamoano ili waweze kuongoza watu vizuri na kwa amani.