Wanawake wanaweza kuongeza uzalishaji

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete

WANAWAKE wanaweza kuongeza kiwango cha uzalishaji na kukuza kilimo katika nchi zinazoendelea iwapo watapewa uwezo wa kumiliki ardhi na kupata mikopo nafuu.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo jijini New York jana (19 Septemba, 2011) wakati wa mjadala juu ya Wanawake na Kilimo, kuzungumzia jinsi ya kuongeza hali ya Usalama wa Chakula Duniani, mjadala uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi Hillary Clinton.
“Wanawake ndio wanaofanya kazi kubwa katika kilimo, lakini hawana sauti kwa kuwa hawamiliki ardhi wala uwezo wa kifedha kuongeza kipato chao”. Rais amesema na kuongeza kuwa, “ili kuondoa hali hiyo, kunahitajika mabadiliko makubwa ya sheria na sera ambazo zitahakikisha wanawake wanamiliki ardhi na pia wanawezeshwa kwa kupewa mikopo”.
Rais amefafanua katika mjadala huo wenye lengo la kuongeza ufahamu na kutilia mkazo suala la wanawake katika kilimo, kutambua mchango wao na kuutambua kuwa moja ya juhudi muhimu katika kuongeza uzalishaji na kuinua kilimo katika nchi zinazoendelea.
Rais Kikwete amesema kutokana na hali halisi ya kiuchumi kwa sasa katika nchi mbalimbali na mabadiliko yanayoendelea duniani ipo haja na ni wakati muafaka wa kutambua juhudi hizo za wanawake na kuzipa nguvu na kwa kutumia elimu, ili kuelimisha jamii juu ya juhudi zinazofanywa na wanawake katika kilimo na umuhimu wa kuzitambua na kuziheshimu juhudi hizo.
Mapema akiwakilisha mada kuhusu Wanawake na Kilimo, Waziri Clinton ametolea mfano wa Rais Kikwete kuwa mmoja wa viongozi katika nchi zinazoendelea ambaye anatilia mkazo kilimo na kusisitiza kutiliwa maanani juhudi za wanawake katika kilimo nchini Tanzania.
“Hili ni suala la kiuchumi, na ni jambo linalowezekana kwani wapo viongozi katika nchi zinazoendelea kama Rais Kikwete, wanaoweka kipaumbele katika kilimo na kutilia mkazo uwezeshwaji wa wanawake na kutambua juhudi zao za uzalishaji, hivyo ni jambo linalowezekana, na hili ni jambo la kiuchumi sio la kijinsia” amesema.
Katika juhudi hizo, Marekani itatoa kiasi cha dola milioni 5 (Dola Milioni Tano) kwa ajili ya kukuza usawa katika kilimo, elimu na utafiti zaidi ili kuwapa uwezo wanawake wengi zaidi na hivyo kuongeza uzalishaji zaidi katika kilimo.
Rais Kikwete yuko jijini New York Marekani kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kila mwaka, ambapo anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 22 Septemba, 2011. Kikao cha Baraza Kuu kinafunguliwa rasmi tarehe 21 Septemba, 2011.
Mbali na Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete anahudhuria mikutano mbalimbali ambayo amealikwa kama Rais wa Tanzania na pia katika nyadhifa zake mbalimbali kama Mwenyekiti wa Jitihada za Viongozi wa Afrika katika Kupambana na Malaria (ALMA).
Rais Kikwete pia ametoa hotuba ya ufunguzi katika mjadala kuzungumzia juu ya Afya ya Meno na Kinywa mjadala uliofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha New York, Kitivo cha Meno.
Mjadala huo umeandaliwa na serikali ya Tanzania kwa kushirikisha nchi za Australia na Sweden.
Mjadala huo umezungumzia kwa kina umuhimu wa kuyapa kipaumbele maradhi yasiyoambukiza lakini yenye uhusiano mkubwa na magonjwa makubwa na yale yanayoambukiza.
Baadaye jioni Rais amepokea Tuzo Maalum Juu ya Afya na Teknolojia ambapo juhudi mbalimbali za viongozi na watu mashuhuri zimetambuliwa kwa kupewa tuzo ya South South.