Wanawake Tofati Zenu za Vyama Zisiwazuie Kushirikiana katika Maendeleo

Mama Salma Kikwete
Wanawake wa mkoa wa Mara wameaswa kushirikiana kwa pamoja katika shughuli za maendeleo bila kuangalia tofauti ya itikadi zao za vyama kwa kufanya hivyo watajiletea maendeleo yao kama wanawake.

Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanawake wa mkoa huo katika ukumbi wa mikutano wa Musoma Community Center (MCC) uliopo mjini Musoma.

Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema masuala yanayowahusu wanawake hayana itikadi za vyama kwani maendeleo ni ya wote, katika mambo ya msingi waungane na kuwa kitu kimoja wasitenganishwe na watu.

Alisema ili wanawake waweze kujiletea maendeleo ni lazima washikamane, wafanye kazi kwa umoja na kutumia fursa zilizopo kwani Serikali inasehemu yake ya kuwaleta maendeleo lakini maendeleo mengine yanahitaji jitihada zao binafsi.

“Sisi kama wanawake tunafanana kwa kila kitu tofauti iliyopo ni wajibu wa kila mmoja wetu katika jamii yake, shirikini kuchangia shughuli za maendeleo kama ujenzi wa barabara na shule kwa ajili ya watoto wetu na kuchangia huduma ya afya ili tuweze kupata huduma bora”.

Msiache kuzitumia fursa zilizopo wasimamieni watoto wa kike wasome kwani wakiwa na elimu wataweza kujiajiri au kuajiriwa, wengine watakuwa viongozi wazuri miaka michache ijayo watawasaidia siku za baadaye”, alisisitiza Mama Kikwete.

Aidha Mama Kikwete alitumia nafasi hiyo kuwaaga wanawake hao na kuwashukuru kwa jinsi walivyokuwa wanamtia moyo katika kipindi chote cha miaka 10 ya utawala wa mme wake Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete jambo ambalo lilimpa ujasiri katika kufanya kazi zake za kuwasaidia wanawake na watoto wa Tanzania.

Mama Kikwete alisema, “Kazi yangu ninayoifanya kama mke wa Rais nimeitekeleza nilisema nitawasomesha watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu nimewasomesha, nimejenga shule ya watoto wa kike, nimewainua wanawake kiuchumi na nimesaidia kuimarisha afya ya mama na mtoto”, alisema Mama Kikwete.

Katika mkutano huo wanawake walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali na kuzitaja kero na changamoto zinazowakabili katika maisha yao kama vile upatikanaji wa maji, uongozi, uchumi na elimu.

Kwa upande wake Theresia Chacha ambaye ni mkazi wa Nyamagugu wilaya ya Rorya alimshukuru Mama Kikwete kwa kumsomesha mtoto wake wa kike aitwaye Paschazia ambaye yupo kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo Rufiji Mkoani Pwani.

“Mama Kikwete anasomesha watoto 15 kutoka mkoa wa Mara katika shule yake, mwanangu ni mmoja wa watoto hao, anamgharamia kila kitu hata nauli mama huyu analipa mimi silipo chochote”.

Miaka yote hiyo sijawahi kumuona ndiyo namuona leo nakushukuru sana Mama, Mwenyezi Mungu akubariki naomba kiongozi ajaye aige mfano wako wa kuwasidia wanawake na watoto wa Tanzania”, Mama Chacha alishukuru.
Naye Anastazia Sangarya mkazi wa kata ya Mwisege ambae ni mjasiriamali alizitaja changamoto wanazokutana nazo kuwa ni pamoja na kupanda kwa ada ya ushiriki wa Maonyesho ya kimataifa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere maarufu kama sabasaba yanayofanyika kila mwaka jijini Dar es Salaam kutoka shilingi 50,000 hadi 100,000.

Mama Anastazia alisema, “Sisi wanawake wajasiriamali tunaumizwa na ada kubwa ya ushiriki wa maonyesho ya sabasaba kwani tukishiriki licha ya kulipa kiingilio bado kuna gharama ya nauli na malazi”.

Kwa upande wa mikopo tunayokopa benki riba yake ni kubwa na kama ikatokea umechelewa kurejesha kutokana na matatizo ya kifamilia benki haikuelewi tunakuomba mama yetu utusaidie kutatua changamoto hizi ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya wanawake wajasiriamali wa mkoa huu,”.

Mama Kikwete aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wanawake hao na kuwataka viongozi wao kuitisha mikutano ya mara kwa mara itakayosaidia kutatua kero zinazowakabili.