Wanawake Sasa Ruksa Kurithi Mali Botswana

Wanawake nchini Botswana

MAHAKAMA Kuu nchini Botswana imebatilisha sheria ya kitamaduni ambayo awali iliwazuia wanawake kurithi mali nyumbani. Kutolewa na uamuzi huo ni neema kwa wanawake nchini humo kwani sasa wataruhusiwa kurithi mali kutoka katika familia zao.

Mahakama imesema kuwa kanuni hiyo ya kitamaduni inakiuka sheria ya katiba inayosisitiza usawa kwa wanaume na wanawake. Taarifa zaidi zinasema, Edith Mmusi na dadake zake watatu walilazimika kwenda mahakamani kutafuta haki hiyo baada ya mpwa wao kusema kuwa yeye ndiye mmiliki wa nyumba yao.

Duru zinasema kuwa wanawake hawaruhusiwi kurithi mali katika jamii nyingi za Kiafrika ingawa katika baadhi ya nchi sheria hizo sasa zinaharamishwa. Mwandishi wa BBC mjini Gaborone, anasema uamuzi wa Jaji Key Dingake, sasa inaileta katika safu moja sheria ya utamaduni na katiba ya nchi.

Alisema kuwa lazima pawepo usawa kati ya wanawake na wanaume kuhusiana na swala urithi. Mmoja wa madada hao waliofika katika mahakama kupinga sheria za kitamaduni , alijawa na furaha isiyo na kifani.
“ni siku nzuri sana kwetu” alisema Mmusi.

Uamuzi wa leo unafikisha kileleni kesi ambayo imekuwa ikiendelea kwa miaka mitano ambayo yeye na madada zake walifikisha mahakamani. Mussi walienda mwanzo katika mahakama za kitamaduni kupinga hatua ya mpwa wao mnamo mwaka 2007.

Lakini walishindwa katika kesi hiyo mara mbili ndiposa wakaamua kwenda katika mahakama ya kiraia.
-BBC