Wanaume wa Tarime Wakataa Ukeketaji

Mamia ya wanawake na wanaume wakiwemo watoto walifurika kusheherekea mafanikio ya harakati za ukombozi wa Mwanamke na kupinga ukatili dhidi ya wanawake Tarime.

Mamia ya wanawake na wanaume wakiwemo watoto walifurika kusheherekea mafanikio ya harakati za ukombozi wa Mwanamke na kupinga ukatili dhidi ya wanawake Tarime.

Washiriki wa Tamasha la Jinsia ngazi ya Wilaya Tarime lililofanywa na TGNP.

Washiriki wa Tamasha la Jinsia ngazi ya Wilaya Tarime lililofanywa na TGNP.

Na Deogratius Temba

WANAUME kutoka katika Kata ya Nyamaraga Kijiji cha Ng’ereng’ere Wilaya ya Tarime mkoani Mara wamewataka wanaume wote kukataa kuoa wasichana waliokeketwa ili kukomesha kabisa mila hizo potofu.

Akizungumza katika Tamasha la Jinsia ngazi ya wilaya lililofanyika katika kata hiyo nje kidogo ya mjini wa Tarime linaloongozwa na TGNP Mtandao, Mchungaji wa Kanisa la PEFA, Getagasembe, Roberty Machera amesema kuwa suala ya ukeketaji linahitaji jamii nzima ya Tarime, wanaume na wanawake kuunganisha nguvu kupambana nalo.

“Tunahitaji mabadiliko ya haraka, wanaume wakatae kwa nguvu zote kuwakeketa watoto wao wa kike na kuoa wanawake waliokeketwa ili tuweze kuua kabisa mila hii kandamizi ambayo inaharibu haki ya msingi ya mwanamke,” alisema mchungaji Machera.

Alisema wanaume wa Tarime wanapaswa kubadilika, na ndio watakao weza kuondoa kabisa mila hiyo kama wanataipinga na kuungana na wasichana wao wanaokataa kukeketwa” mimi ni mwanamke mkuria kama nitasema nakataa binti aliyekeketwa  itakomesha kabisa kwasababu hata wale wanawake wanaopenda kukeketwa watakataa na kuunganisha nguvu nasi,” aliongeza

Kwa upande wake Meneja wa Idara ya Utafiti, uchambuzi na ushawishi TGNP, Mary Nsemwa alisema kuwa wananchi wa Tarime ni lazima kuachana kabisa na mila hiyo na kuondoa dhana ya kufikiri kuwa utajiri wa mali utatokana na kukeketa wasichana na kuwaoza kwa umri mdogo. “achaneni kuwatumia wasichana kama vyombo vya starehe, kujichumia mali, Tarime ni sehemu yenye utajiri wa ajabu, ardhi nzuri yenye rutuba, maji, madini, misitu, hali ya hewa nzuri, tutumie rasilimali hizo kujipatia utajiri lakini sio wasichana,” alisema Nsemwa.

Tamasha hilo linaendeshwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Taarifa na Maarifa Nyamaraga, na kushirikisha mashirika mengine kama Oxfam, Kivulini, na wanaharakati wengine wanaofanya kazi na TGNP kutoka wilaya za Kishapu, Mbeya vijijini, Morogoro Vijijini, na Kinondoni Dar es Salaam.