Wanasiasa Tanzania Wahusishwa na Mauaji ya Albino!

Bi. Grace Medaldi kama alivyonaswa na Huffington Post.

Bi. Grace Medaldi kama alivyonaswa na Huffington Post.

Katika makala iliyopewa jina la “Love in a Time of Fear: Albino Women’s Stories From Tanzania”, iliyorushwa kwenye gazeti la intaneti la Huffington Post (tarehe 25/10/2013 na kuhuwishwa tena tarehe 23/01/2014) kutoka Marekani, ililbaini kwamba wanasiasa wa Tanzania wanahusishwa na mauaji ya albino, na kipindi cha uchaguzi ndio kipindi hatari kwa maisha ya albino nchini. Kuhusishwa huko kwa wanasiasa wa Tanzania, almaarufu kama “Bongo”, kuligundulika (bila shaka, sio kwa mara ya kwanza) baada ya Chika Oduah, muandishi wa makala hayo, kutembelea Bongo na kufanya mahojiano na wanawake kadhaa  maalbino.

Mmoja wa wanawake hao aliyefahamika kama Grace Medaldi (pichani juu), ambaye mpaka makala yanaandikwa alikuwa anaishi Moshi kwenye kituo maalum (kwa usalama wake), akitokea Sumbawanga, alisema kipindi anacho ogopa zaidi katika maisha yake Bongo ni kipindi cha uchaguzi. Grace aliweka wazi kwamba kipindi cha uchaguzi, ni kipindi ambacho watu (wagombea na wapambe wao) wana amini kwamba wakiua albino au wakipata sehemu ya viungo vya mwili wake, basi watashinda uchaguzi. Oduh aliweza pia kusikia baadhi ya wakazi wa maeneo mbalimbali aliyotembele wakisema kwamba wanasiasa hupanga mauaji ya albino na kushirikiana na waganga, ili mambo yao yaende sawa kwenye uchaguzi. Habari za mjini ni kwamba kiungo kimoja cha ndugu zetu albino kinaweza kumgharim mteja mpaka $2,000.

Ndugu zangu, nimeona kuna umuhimu wa kujikumbusha uchunguzi wa makala haya ya Bi. Oduah, kwani kama tujuavyo nchi yetu inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge, na madiwani mwishoni mwa mwaka huu na mpaka sasa vikumbo mbalimbali vinaendelea kwa wale wanaoutaka urais, ubunge, na udiwani kupitia vyama mbalimbali nchini, lakini haswa haswa chama tawala. Wakati hayo yakiendelea, hivi karibuni kama tulivyosikia yule binti albino aliyetekwa, alikutwa kafa huku akiwa hana mikono wala miguu. Pamoja na tukio hili la kinyama, la aibu, na kusikitisha, matukio mengine ya ajabu ajabu dhidi ya albino yamekuwa yanaendelea nchini mwetu Tanzania, nchi ambayo wengi wanataka tuamini au wanaamini kwamba “ni kisima cha amani na utulivu”. Katika hali kama hii kweli tunajivunia amani ya aina gani? Kwa mujibu wa makala ya Oduah, Umoja wa Mataifa (UN) tayari umeiweka Tanzania katika nafasi ya juu linapokuja suala la mauaji ya albino. Pia, mbali na kuwa kwenye list ya juu, Tanzania inalaumiwa kwa kuwa na namba ndogo ya watu waliohukumiwa kwa mauaji ya albino, kwani katika idadi ya mauaji 72 yaliyoripitiwa tokea mwaka 2000, ni watu watano tu ndio waliotiwa hatiani.

Mpaka sasa sioni kama serikali na wanasiasa wamefanya juhudi za kutosha kuhakisha kwamba ndugu zetu albino wanalindwa na kuheshimiwa kama binaadam wengine na hii inahashiria kwamba tuhuma (na tayari shuhuda mbalimbali zina shawishi hivyo) zinazoelekezwa kwao kwamba wanasiasa ndio wateja wakubwa wa imani hizi za kishirikina, ni za kweli. Baada serikali kujitutumua na kupiga marufuku waganga wa kienyeji na ramli, muandishi Evarist Chahali, alisema “Amri ya serikali kupiga marufuku waganga wa kienyeji na ramli ni ya kipuuzi, kwa sababu kama serikali hiyohiyo inashindwa kuwadhibiti mafisadi wanaokwapua mabilioni sehemu kama Benki Kuu penye CCTVs lukuki itawezaje kuwabana waganga na wapiga ramli wanaofanya shughuli zao kwa siri?“.

Chahali ana haki zote za kutokuwa na imani na tamko hili la serikali, na ili serikali ilirudishe imani kwa tulio wengi tunaofuatilia ufanyi kazi wa serikali yetu, basi lazima ituonyeshe kwamba haitoishia kwenye kupiga marufu tu, bali pia inafanya vitendo. Serikali kwa kushirikiana na wenyeviti wake wa miji na vijiji (siku hizi wanatoka vyama mbalimbali vya siasa) pamoja na viongozi wengine wa ngazi tofauti, washirikiane kuweka mitego ya kisayansi, ili kubaini waganga, ambao sio tu wanaendelea  na shughuli zao, bali wale haswa wanaotoa masharti ya kuletewa viungo vya albino, ili kufanikisha mambo.

Ninaposema “mtego wa kisayansi” namaanisha kama ile mitego inayofanywa Nigeria kubaini madaktari na mafamasia feki, wanaouzia watu dawa wasiozihitaji, yaani mtu anaambiwa ana ugonjwa ambao hana, halafu anauziwa dawa ambayo haihusiani na ugonjwa na wala huo ugonjwa haupo. Au mitego kama ile inayofanywa Kenya na kile kipindi cha “Jicho Pevu”. Kwa ufupi, lazima kuwe na mkakati maalum, utakao fadhiliwa na kisimamiwa na serikali bila kumuonea aibu mtu yeyote, ili kuhakikisha albino wanaishi kweli katika nchi ya “amani na utulivu”. Bila mkakati maalum, na kuhakikisha kwamba wote wanaokamatwa wanafikishwa kwenye vyombo husika na kuchukuliwa hatua, basi ni dhahiri kwamba hizi nazo zitakuwa ni porojo tu kama porojo nyingine tulizozizoea.

Rungwe Jr.

www.thehabari.com

Kama unataka kusoma article ya Chika Oduah, iliyonukuliwa hapa, unaweza ukagonga: http://www.huffingtonpost.com/chika-oduah/love-in-a-time-of-fear_b_4154057.html