Wanaopinga ubunge wa Lema wampeleka mahakamani

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA)

Na Janeth Mushi, Arusha

KESI ya kupinga matokeo ya Ubunge dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), inatarajiwa kuanza kusikilizwa Jumatatu mbele ya Jaji Aloyce Mujulizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Habari za ndani kutoka mahakamani hapo zinasema kuwa waliofungua kesi hiyo ni Musa Hamisi Mkanga na wenzake dhidi ya Lema na Mwanasheria wa Serikali, katika kesi ya madai namba 13 ya 2010.

Katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana, Lema alimshinda kwa kura nyingi aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira), Dk. Batilda Burian ambaye alikuwa mshindani wake wa karibu kwa tofauti ya kura 56,196 huku Burian akiambulia kura 37460.

Aidha katika hauta nyingine Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa
imeahirisha kesi iliyofunguliwa na madiwani watano wa CHADEMA
waliofukuzwa uanachama hadi Septemba 9 mwaka huu, ambapo mapingamizi manne yaliotolewa na upande wa utetezi yatakapoanza kisikilizwa.

Wakili wa upande wa utetezi unaoongozwa na Metod Kimomogolo na Albert Msando, ulidai kuwa Mahakama hiyo Haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kuitaja Mahakama Kuu ndiyo inaweza kuisikiliza.

Kimomogolo amedai pingamizi la pili ni kupinga, Freeman Mbowe
kushitakiwa binafsi katika kesi hiyo, CHADEMA hakiwezi kushitakiwa kwa jina lake na pia kesi hiyo imepitwa na wakati kwa kuwa maombi hayo ya kupinga yameshawasilishwa Baraza Kuu la CHADEMA na madiwani hao ambapo bado haijaanza kusikilizwa.

Awali kabla ya kuahirisha shauri hilo Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo
Hawa Mguruta alikubaliana na maombi ya pande zote mbili ya kuahirishwa kwa kesi hiyo hadi hapo Ijumaa, mahakama hiyo itakapoanza kusikiliza pingamizi hizo nne(4).

Madiwani hao wanatetewa na Wakili, Severine Luwena, wakati Chadema na Freeman Mbowe wanatetewa na mawakili Method Kimomogolo na Albert Msando. Madiwani hao ni Estominh Mallah, Charles Mpanda, John Bayo, Rehema Mohammed na Reuben Ngowi ambao wanatetewa na wakili Severine Luwena.