Na Beatrice Lyimo – Maelezo.
BARAZA la Tiba Asili na Tiba Mbadala latoa tamko kuhusu vipindi na matangazo yote ya tiba asilia na tiba mbadala yanayoonyeshwa kwenye vyombo vya habari hapa nchini kuwa ni batili yenye kupotosha na yasiyo na vibali.
Akizungumza na waandishi leo jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Baraza hilo Profesa Rogassian Mahunnah alisema kuwa, baraza hilo linawashauri wananchi kutoamini huduma zinazotangazwa na watu hao kuhusu tiba wanazozitoa. Alisema kuwa, kwa mujibu wa Sheria shughuli zote zinazohusu tiba asilia na tiba mbadala ni budi zisajiliwe na kupewa kibali kutoka Baraza la Tiba Asili na Tiba mbadala.
“Kanuni za maadili, miiko na mienendo ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala, imeweka utararibu wa kufuatiliwa pale mganga wa tiba asili na tiba mbadala anapotangaza shughuli zake kupitia vyombo vya habari na mabango kwa jamii” alisema Profesa Mahunnah.
Kwa mujibu wa taarifa za Mwenyekiti huyo zinasema kuwa, kumekuwa na uwepo wa Maafisa feki wakijitambulisha kama Maafisa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii na kutoa vibali bandia kwa njia ya simu kuhusu urushwaji wa vipindi katika vyombo vya habari.
Naye kaimu Msajili wa Baraza hilo, Bi. Mboni Bakari ameongeza kuwa, kumekuwepo pia na matumizi ya mashine ya Quantum na za kuondoa sumu mwilini kwa baadhi ya waganga ambao hawana elimu ya kutosha juu ya kutafsiri majibu na kujua matumizi sahihi ya vifaa hivyo.
“kutokana na kutosajiliwa kwa mashine hizi na TFDA, ufanisi na usahihi wa mashine ya kuondoa sumu mwilini hautambiliki na hauna uhakika,” aliongeza Bi. Mboni.
Aidha, Baraza hilo linawasisitizia waganga kuendelea kufanya usajili kwenye ofisi za waratibu wa tiba asilia na tiba mbadala katika Wilaya na Halmashauri zao na kutoa huduma katika sehemu walizosajiliwa.