‘Wananchi Wanataka Uadilifu na Uaminifu si Majengo Mazuri’

Rais Jakaya Kikwete akiteta jambo na baadhi ya Mawaziri aliofuatana nao katika ziara yake ya kuutembelea Mkoa wa Njombe wakati aliposimama katika kijiji cha Kipengere huko Wanging’ombe kukagua mambo ya maendeleo na pia kusalimiana nawananchi tarehe 19.10.2013. (PICHA NA JOHN LUKUWI)  

Rais Jakaya Kikwete akiteta jambo na baadhi ya Mawaziri aliofuatana nao katika ziara yake ya kuutembelea Mkoa wa Njombe wakati aliposimama katika kijiji cha Kipengere huko Wanging’ombe kukagua mambo ya maendeleo na pia kusalimiana nawananchi tarehe 19.10.2013. (PICHA NA JOHN LUKUWI)  

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa majengo mazuri ya ofisi za Halmashauri mbali mbali nchini ni muhimu lakini muhimu zaidi ni wafanyakazi na watumishi wa halmashauri hizo kuwa waaminifu na waandilifu katika utumishi wa umma.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa watumishi wa halmashauri nchini kupunguza manung’uniko na malalamiko ya wananchi kwa kutimiza ipasavyo wajibu wao wa kutumikia wananchi.

Rais Kikwete ameyasema hayo Oktoba 20, 2013, wakati alipoweka jiwe la msingi kwenye Ujenzi wa Jengo la Halmashauri ya Mji wa Njombe kwenye eneo la Mji Mwema, nje kidogo ya mji wa Njombe.

Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya siku saba ya kikazi katika Mkoa wa Njombe amewaambia wananchi na viongozi waliohudhuria sherehe hizo ya kuweka jiwe la msingi:

“Nawapongezeni kwa kujenga jengo zuri na jipya kama hili. Linaongeza heshima kwa mji wa Njombe ambao ni makao makuu ya Mkoa wa Njombe. Lakini ubora wa jengo pekee hautoshi kwa utumishi bora wa wananchi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Ubora wa utumishi wa wananchi utapatikana tu endapo watumishi wa halmashauri hii na nyingine zote nchini watakaofikia kiwango cha kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu,wenye tija na matunda ya dhahiri kwa wananchi.”

Rais Kikwete amesema kuwa moja ya wajibu mkubwa wa watumishi wa halmashauri na wa umma kwa jumla nchini ni kupunguza malalamiko na manung’uniko ya wananchi kwa kuboresha kiwango cha ubora wa utumishi wao.

Sheria hii ya Manunuzi itatuua, VETA yamwambia Rais Kikwete
Wakati huo huo; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na serikali yake wameombwa na Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi (VETA) nchini kuangalia upya na kwa haraka, umuhimu wa kuifanya marekebisho Sheria ya Manunuzi nchini kwa sababu sheria hiyo katika hali yake ya sasa inarudisha nyuma maendeleo ya VETA na taasisi nyingine nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Eng. Zebadayo Moshi amemwambia Rais Kikwete, Oktoba 19, 2013, kuwa ni vigumu kwa VETA kulazimika kwenda makampuni ya Toyota ama Scania kila mara kununua magari mapya kwa ajili ya mafunzo ya wanafunzi wao kwa sababu Sheria hiyo inazuia taasisi za umma kununua na kutumia vifaa vilivyokwishatumika.

Mkurugenzi huyo alikuwa akizungumza leo kwenye Sherehe ya Ufunguzi wa Kituo cha Mafunzo ya Ufundi cha Wilaya ya Makete (MDVTC) cha VETA, mjini Iwawa, mji mkuu wa Wilaya ya Makete, ambako Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi na ambaye amefungua rasmi Kituo hicho.

Amesema Eng. Mosha: “Sheria hii ya manunuzi itaua kabisa shughuli za VETA na taasisi nyingine za umma nchini. Sisi siku zote, tunafundisha kwa vitendo na hivyo tunapotaka kumfundisha mwanafunzi gari ni lazima tuwe na gari ama jinsi injini ya gari inavyofanya kazi ni lazima tuwe na injini. Lakini kwa sababu Sheria hii inatuzuia kununua vifaa vilivyotumika, tunalazimika kwenda Toyota ama Scania kununua gari jipya ama injini ya gari mpya. Hili litatufikisha mbali kweli?”

“Majuzi tumeanzisha mafunzo ya ndege na injini za ndege zinavyofanyakazi na kwa sababu ya Sheria hii ni lazima twende Kampuni ya Boeing ya Marekani kununua injini ya ndege hiyo,” amesema kuwa wananchi walioshiriki sherehe hiyo wakiangua vicheko.

Rais Kikwete amemwambia Mkurugenzi Mkuu huyo wa VETA: “Nimesikia. Tutazungumza na wahusika kuona nini kinaweza kufanyika. Tulipata kujaribu kuifanyia marekebisho sheria hii lakini wakubwa wale wakakataa na kuruhusu taasisi moja tu ya Serikali kuweza kununua vifaa vilivyokwishakutumika.”

Kituo hicho cha Ufundi cha VETA cha Wilaya ya Makete ni cha kwanza cha aina yake kujengwa nchini kwa sababu ni cha kwanza kujengwa kwa dhana ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM mwaka 2013 ambayo iliahidi kuanza kujenga vyuo vya ufundi katika wilaya badala ya mikoa.

Aidha, Kituo hicho ni cha kwanza cha aina yake nchini kwa kuwa kimejengwa na wanafunzi na wakufunzi wa Chuo cha VETA Mpanda, Mkoa wa Katavi, jambo ambalo limeokoa gharama za ujenzi kwa kiasi cha Sh. bilioni 1.45 pamoja na kwamba mchanga wa ujenzi uliokuwa unachukuliwa kutoka Makambako, mji mwingine wa Mkoa wa Njombe kwa sababu Makete hakuna mchanga unaofaa kwa ujenzi wa mithili ya chuo hicho.

Chuo hicho ambacho ujenzi wake ulianza Aprili 27 mwaka huu kwenye eneo la Kituo hicho la ekari 124 tayari kina wanafunzi 37 wanaoshiriki mafunzo ya ufundi ya ushonaji na uashi wakiwa ni miongoni mwa wanafunzi 145,511 ambao wanaendelea na mafunzo katika vyuo vya ufundi pote nchini.

Akizungumza na wananchi baada ya kufungua Kituo hicho cha kisasa na cha kuvutia, Rais Kikwete ameipongeza VETA kwa kujenga chuo hicho cha kwanza kwa dhana mpya ya kufikisha elimu ya ufundi wilayani.

Rais Kikwete pia ameitaka VEAT kuendelea kutoa mafunzo kulingana na mahitaji ya eneo husika na kutumia raslimali zinazopatikana katika eneo ambako chuo kipo na kwa Mkoa wa Njombe amesema kuwa anataraji kuwa VETA itajiekeleza katika ufundi unaohusiana na mazao ya mbao na wa viazi mviringo.
“Uhodari wa watu wa Makete hauwezi kuendelea kuwa kupanga viazi ama mbao tayari kuzipeleka sokoni Dar Es Salaam, Uhodari sasa uwe ni wa kuanzisha viwanda vya fenicha baada ya vijana wenu kupata mafunzo katika Kituo hiki ama kutengeneza mapochopocho yanayotokana na viazi. Tunahitaji siku moja na sisi kusema kuwa fenicha hii safi imetengenezwa Makete.”

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa VEAT iangalie uwezekano wa kuwapatia wahitimu wake zana na vifaa vya kuanzia kazi za kujitegemea baada ya kumaliza mafunzo yao. “Lazima vijana hawa tuwasaidie kujiajiri kwa sababu tunahitaji sana mafundi stadi na mafundi mchundo kuongeza thamani kwenye uchumi wetu.”