*Maandamano yaendelea, askari waliouwa wanahojiwa
Na Mwandishi Wetu, Songea
BAADHI ya Wananchi wa Manispaa ya Songea wamewakamata vijana wawili wanaowahisi ni miongoni mwa wanaofanya mauaji ya kikatili jioni majira ya saa kumi na mbili na nusu jana eneo la Mkuzo, kisha kuwashambulia kwa kipigo na kuwapeleka kwa maandamano hadi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakidai huo ni ushahidi wao.
Taarifa ambazo mtandao huu umezipata ni kwamba matukio ya mauaji sasa yamehamia Wilaya ya Mbinga na usiku wa kuamkia jana mtu mmoja amechinjwa, huku taarifa zikidai na Songea Mjini tena eneo la Luhuwiko amechinjwa mwingine mwingine usiku wa kuamkia jana katika mazingira hay ohayo ya mauaji.
Baada ya tukio hilo wananchi walianzisha maandamano mengine kuonesha kukerwa na kitendo hicho lakini hadi taarifa hii inatumwa hali haikuwa mbaya, lakini polisi walilazimika kuwatawanya waandamanaji.
Hata hivyo haikuweza kuthibitisha watuhumiwa waliopigwa kweli ni miongoni mwa wauaji wa kikatili japokuwa, wananchi walivyo wahoji maelezo yao yalikuwa na utata.
Juzi maandamano makubwa yalifanywa na Wananchi Wilaya ya Songea wakipinga matukio ya mauaji mfululizo yanayodaiwa kuhusishwa na imani za kishirikina ya uchimbaji wa madini ya uraniamu eneo la Namtumbo na nje ya nchi.
Jeshi la Polisi Wilayani Songea liliwapiga risasi na kuwauwa waandamanaji wawili wakiwa likipambana na waandamanaji ili kuwatawanya waliokuwa wakitokea maeneo mbalimbali ya wilaya ya Songea kuelekea Hospitali ya Wilaya na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Taarifa zinasema hadi sasa watu wanaokadiriwa 14 wameuwawa kikatili na kuondolewa baadhi ya viungo vya sehemu za siri huku taarifa ambazo hazijathibitishwa zikidai vinatumika katika matambiko kwenye migodi ya Uraniamu huko Namtumbo. Hata hivyo polisi inasema ni watu wanane tu ndiyo wamekwisha uwawa hadi sasa na watuhumiwa wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka yao.
Wakati huo huo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Michael Kamhanda ameviambia vyombo vya habari kuwa Jeshi hilo limewashikilia askari wake wanne huku likiwahoji ambao ndiyo wanaotuhumiwa kufyatua risasi na kuwauwa waandamanaji wawili. Akifafanua alisema hizo ni taratibu za kawaida za kuwahoji wajieleze kwanini walitumia risasi na kuangalia kama walilazimika kufanya hivyo. Alisema pia tume itaundwa na kuwahoji na baada ya uchunguzi huo taarifa itawekwa hadharani.