WANANCHI wa kata ya Mpambala, wilaya ya Mkalama mkoani Singida wameiomba Serikali kuhakikisha inamaliza ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti haraka iwezekanavyo ili kurahisisha huduma za mawasiliano kati ya wilaya ya hiyo na mikoa jirani ya Simiyu, Manyara na Mara.
Wananchi hao wamemweleza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, alipofika kukagua daraja hilo mkoani humo jana, ambapo pamoja na mambo mengine wamesema kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutatatua changamoto za usafiri hususan katika kipindi cha masika.
“Tunaomba Mheshimiwa Naibu Waziri utusaidie kukamilisha daraja hili mapema ili tupate huduma muhimu kama usafiri hasa kipindi cha masika”, amesema mmoja wa wananchi.
Aidha, wananchi hao wameipongeza Serikali kwa kuendelea na jitahada za ujenzi wa barabara za maingilio zenye urefu wa KM 25 katika daraja hilo ambapo kwa sasa mradi wote umefika asilimia 43.9.
Kwa upande wake Naibu Waziri Eng. Ngonyani ameuagiza Uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoani humo kuhakikisha kuwa wanamsimamia mkandarasi na kuhakikisha anamaliza ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara hizo kufikia mwezi Machi mwakani.
Kuhusu deni la mkandarasi huyo analoidai Serikali, Eng. Ngonyani amesema kuwa watahakikisha wanamlipa mapema ili kufanikisha mradi kumalizika kwa muda uliopangwa.
“Tutahakikisha tunalipa deni lote linalodaiwa ili kurahisisha mradi huu kuisha haraka kwa ajili ya wananchi kuweza kutumia daraja hili pamoja na barabara yake kwa kuwa ni kiungo muhimu kwao,” amesisitiza Naibu Waziri.
Ametoa rai kwa wananchi wa maeneo hayo mara tu mradi unapomalizika kuhakikisha wanalinda miundombinu yake kwani Serikali inatumia gharama kubwa katika utekelezaji wake. Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoani humo, Eng. Yohanes Mbegalo, amemuahidi Naibu Waziri huyo kuwa atahakikisha mradi huo unaisha kwa wakati ili kuwaondolea wananchi kero ya usafiri.
Daraja la Sibiti lenye urefu wa mita 82 linajengwa na mkandarasi China Hanan ambalo linatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwakani na kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 16.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano