Wananchi waanza kuunusuru Mlima Kilimanjaro

Kilele cha Mlima Kilimanjaro

Na Mwandishi Wetu, dev.kisakuzi.com-Moshi

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amesema mkoa huo umeanza kampeni ya upandaji miti katika maeneo anuai ikiwemo kwenye vyanzo vya maji, mito na kingo za mito na lengo ni kupanda miti milioni 8 kwa mwaka huu pekee.

Gama ameyasema hayo leo kwenye uzinduzi wa kampeni za upandaji miti katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, na kuongeza kuwa nia ni kuhakikisha Kilimanjaro inakabiliana na uharibifu wa mazingira sanjari na kurejesha uoto wa asili na theluji ya Mlima Kilimanjaro ambayo imeanza kuyeyuka na kuleta athari kwa wakazi wa maeneo hayo.

Kiongozi huyo alisema ili kufikia malengo yaliyowekwa halmashauri za wilaya mkoani Kilimanjaro hazina budi kusimamia sheria za misitu na upandaji miti na kudhibiti wale wate watakaobainika kukiuka sheria na taratibu.

Ameongeza suala la upandaji miti ni jukumu la kila mwananchi, hivyo ni vema viongozi wa halmashauri wakatoa elimu kwa wananchi ili kuanzisha vitalu vya miti katika kata, mitaa na vijiji. Uanzishwaji vitalu utasaidia ongezeko la idadi ya miti itakaopandwa kipindi cha mwaka ujao hivyo kufikia malengo.

“Mkoa wa Kilimanjaro tumepanga kupanda miti milioni Nane katika kipindi cha mwaka huu, lengo ni ili kuweza kukabiliana na uharibifu wa mazingira ambao umeleta madhara makubwa katika jamii na mkoa wetu wa Kilimanjaro kwa ujumla,” alisema Gama.

Awali akizungumza Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Bernadetha Kinabo alisema katika kipindi hiki cha mvua za masika na vuli wanatarajia kupanda zaidi ya miti milioni 1.6 katika maeneo ya makorongo, kingo za mito na hifadhi za bararaba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo kila mwananchi atalazimika kupanda miti 8 kwa mwaka huu.