Na Florah Temba
WANANCHI wa Kijiji cha Matadi Kata ya Ndumeti wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wameondokana na Adha ya kutembea Umbali wa zaidi ya Kilomita 10 kutafuta Huduma za umeme, baada ya kufungiwa Mtambo wa nishati ya Umeme inayotumia Mafuta ya Mbono(Jatropha) na Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na Nishati endelevu na Utunzaji wa Mazingira Tanzania (TATEDO) kwa ufadhili wa jumuiya ya umoja wa Ulaya.
Akizungumza mara baada ya kufunguliwa kwa Mtambo huo Mratibu wa Mradi wa nishati ya umeme vijijini Katika shirika la TaTEDO Bw. Shukuru Meena alisema shirika hilo limeguswa kutoa Mtambo huo ambao umefungwa kitongoji cha mjimwema katika kijiji hicho baada ya kuona wananchi wanapata shida ya umeme.
Alisema kupitia Mtambo huo Wananchi wa maeneo hayo wataweza kuendesha shughuli mbalimbali za kimaendeleo na za kuwaongezea kipato pamoja na kupata mwanga hatua ambayo itawasaidia kukabiliana na gharama kubwa za Mafuta ya taa na kujikwamua kiuchumi.
Alisema Mtambo huo utaweza kuendesha Mashine ya kusaga,kukoboa na kuchuja Mafuta ya Mbono pamoja na kuchaji Betry mbalimbali zikiwemo za magari na Sola hatua ambayo itawawezesha Wananchi kunufaika na mwanga na hivyo kuendesha shughuli mbalimbali za kimendeleo hadi nyakati za usiku.
Aidha alisema Shirika hilo lina Mpango wa kufunga Mtambo kama huo Wilaya ya Hai na Mwanga mkoani Kilimanjaro,Muheza na Lushoto mkoani Tanga,Meru,Monduli na Karatu mkoani Arusha, Kahama, Misungwi na Geita pamoja na maeneo mbalimbali nchini ambayo hayajafikiwa na Umeme wa Gridi ya Taifa, lengo likiwa ni kuwawezesha Wananchi kunufaika na Nishati ya umeme na kujikwamua kiuchumi kupitia nishati hiyo.
“Tuna mpango wa kufunga mitambo 50 kama hii maeneo mbalimbali nchini ambayo hayajafikiwa na umeme wa gridi ya Taifa, na lengo letu hasa ni kuwawezesha Wananchi kujikwamua kiuchumi,na Mitambo hii tutakayoifunga itakuwa inasimamiwa na Wananchi wenyewe na huu tulioufunga hapa utasimamiwa na kikundi cha Benk Imani kilichopo hapa kijijini ambacho Wananchi wameona ndicho kitawezakusimamia” alisema.
Alisema katika ufungaji Mitambo hiyo mingine watawatumia Vijana wenye fani ya utengenezaji Magari na uchomeleaji Vyuma kutoka wilaya mbalimbali Nchini ambao wamepatiwa Mafunzo kwa muda wa wiki mbili wilayani siha lengo likiwa ni kuwawezesha kupata Ujuzi na kuweza kwenda kufanya kazi hiyo katika wilaya zao pindi watakapofikiwa ikiwa ni moja ya Ajira na kujiongezea kipato.
Mratibu huyo alitumia Nafasi hiyo kuwataka Wakulima Nchini kuhamasika kulima kilimo cha Mbono ambacho kwa sasa kina Soko kubwa ndani na nje ya Nchi hatua ambayo itawawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na hali ya utegemezi katika Jamii.
Wakizungumza baadhi ya Wananchi waliofikiwa na Huduma hiyo walilishukuru shirika hilo na kusema kuwa kwa sasa wanaweza kufanya shughuli mbalimbali za kuwaongezea Kipato ikiwemo Biashara kwa muda mwingi hata Usiku tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wanalazimika kufunga Biashara zao saa kumi na mbili jioni kutokana na kuwepo kwa Giza nene.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wilayani Siha Bw. Gilliard Mmari akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa wilaya hiyo Bw.Rashid Kitambulio alisema kuwekwa kwa Mtambo wa umeme katika kijiji hicho kutasaidia uharakishaji wa ukuaji wa Maendeleo ikiwa ni pamoja na kukuza kiwango cha Taaluma kutokana na kwamba Wanafunzi wengi hasa wa kipato cha chini walishindwa kujisomea nyakati za Usiku kwa kushindwa kumudu gharama za Mafuta ya taa