Wananchi: Tafiti za utawala bora za APRM zifanyiwe kazi

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe akifurahia jambo na Ofisa Habari wa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) Tanzania, Bw. Hassan Abbasi kwenye wakati Waziri huyo alipotembelea banda la APRM juzi. APRM ni miongoni mwa taasisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa zinazoshiriki maonesho ya Wizara hiyo katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru. Picha na Mpiga Picha Maalum.

Na Mwandishi Wetu

Wananchi wa kada mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali jijini Dar es Salaam wamesema katika kuboresha na kuinua utawala bora nchini miaka 50 ijayo ni vyema Serikali ikafanyiakazi tafiti mbalimbali zinazofanywa na taasisi zake hasa tafiti za utawala bora zinazofanywa na APRM.

Wananchi hao walitoa maoni hayo kwa nyakati tofauti walipotembelea banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Maonesho ya Wiki ya Wizara hiyo kwa ajili ya miaka 50 ya uhuru yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

APRM ni Mpango wa Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora na hapa nchini taasisi hiyo imepewa dhamana ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu hali ya utawala bora ili kuisaidia Serikali kufanyiakazi changamoto zinazojitokeza.
“Nimesikia kuhusu utafiti wenu na hasa kuhusu namna nchi yetu inavyojenga uelewa wa wananchi ili waseme utawala bora wanaoutaka,”alisema mmoja wa wananchi waliohudhuria banda la APRM.
Wananchi wengine walihoji kutaka kueleweshwa watashiriki vipi katika mchakato huo huku wengi zaidi wakionesha wasiwasi kama taasisi hiyo imetangazwa vya kutosha ili kuwapa nafasi wananchi na kama maoni yao yatafanyiwakazi.
Akifafanua baadhi ya kero za wananchi, Ofisa Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania, Bw, Hassan Abbas alisema mchakato huo ulipoanza nchini wananchi walielimishwa kupitia mikutano iliyofanyika hadi vijijini na pia kupitia semina za makundi na vyombo vya habari na uelimishaji zaidi unaendelea.
“Kuhusu Serikali kufanyiakazi maoni ya wananchi hilo sisi bado hatujafikia hatua hiyo maana katika mchakato huu baada ya Rais kuwasilisha ripoti mbele ya wakuu wenzake wa Umoja wa Afrika ndipo anapewa michango kisha nchi inaanza kufanyiakazi maoni ya wananchi kwa miaka mitatu kabla ya kufanyika tena utafiti mwingine,” alisema na kuongeza kuwa utekelezaji wa maoni hayo unaweza kuanza mwakani.

Aliongeza kuwa hata hivyo kabla ya hatua hiyo kufikiwa nchi haizuiwi kuanza kufanyiakazi maoni ya wananchi wake yaliyotolewa katika ripoti. “Hapa nchini ukiangalia maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu masuala kama katiba na matakwa ya kudhibitiwa matumizi holela ya fedha katika chaguzi, haya yameshaanza kufanyiwa kazi au yanaendelea kufanyiwa kazi,” alisema Bw. Abbas.