Na Joachim Mushi, dev.kisakuzi.com Kishapu
SHIDA ya maji inayoikabili Wilaya ya Kishapu imeendelea kuwabebesha wananchi mzigo pasipo kutarajia, hasa wagonjwa kwani kwa sasa wananchi wa Mji mdogo wa Maganzo Kata ya Songwa wanalazimika kwenda kutibiwa wakiwa na madumu ya maji kulingana na huduma anayoita muhusika.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi mjini hapa, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Maganzo, Lwinzi Kidiga alisema wamewaelekeza wananchi kwenda kutibiwa huku wakiwa na maji kwenye madumu ili kuiwezesha Zahanati ya Maganzo kuendesha shughuli zake kwani hakuna maji katika kituo hicho.
Alisema wananchi eneo hilo hulazimika kwenda na maji kati ya madumu (ya lita 20) mawili hadi matatu kulingana na uhitaji wa maji katika huduma ambayo mgonjwa anastahili kupata jambo ambalo amekiri kuwa ni kero kwa wananchi wake.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini licha ya wananchi kulazimika kuja na maji katika zahanati hiyo pia wanapokuja kupata huduma za afya usiku hulazimika pia kuja na mafuta ya taa au tochi ambayo hutumika kuangaza wakati mgonjwa akipatiwa huduma, kwani zahanati hiyo haina umeme.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Lucas Said akizungumza na mwandishi wa habari hizi amekiri kuwepo na utaratibu wa kuwatoza maji wananchi wanaokwenda kupata huduma za afya na kudai tatizo la maji lipo kwa zahanati nyingi za eneo hilo na juhudi zinafanywa kuhakikisha huduma ya maji inapatikana maeneo anuai ya Kishapu.
Alisema kwa sasa wataalamu wanafanya utafiti katika vijiji mbalimbali kuhakikisha vinapatiwa huduma ya maji pale mpango wa kuleta maji kutoka Ziwa Victoria kwa matumizi eneo hilo utakapo kamilika. Hata hivyo ameshauri watendaji katika zahanati na vituo vya afya kuhakikisha wanajipanga vizuri katika matumizi ya fedha za ruzuku ili ziweze kugharamia huduma kama hizo na kuondoa usumbufu kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Maganzo, Kidiga ilipo zahanati hiyo amesema tayari uongozi wa kijiji umefanya mazungumzo na mwekezaji wa madini ya almasi eneo hilo, mmiliki wa mgodi wa Williamson unaochimba almasi eneo hilo kuwaletea maji wananchi mradi utakaoanza kati ya mwezi Julai mwaka huu.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa dev.kisakuzi.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).