Na Mwandishi Wetu, Siha
WANANCHA wilayani Siha mkoani Kilimanjaro wamesema watagoma kutoa maoni ya uundwaji wa Katiba mpya endapo hawata elimishwa kwanza juu ya katiba iliyopita na mambo mengine muhimu ndani ya katiba.
Wamesema Katiba iliyopo ya Mwaka 1977 hawaifahamu kabisa hivyo watashindwa kuchangia maoni ya mabadiliko ya Katiba mpya kutokana na kwamba hawafahamu hata ni maeneo gani yanaweza kuhitaji mabadiliko.
Akizungumza, Erasto Mbise mkaazi wa kata ya Gararagua wilayani Siha alisema pamoja na serikali kuunda tume ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba, wananchi wengi hususani wa maeneo ya vijijijni hawaielewi katiba iliyopo ambayo inahitajika kufanyiwa marekebisho.
“Tunaipongeza sana serikali kwa kuunda tume ya kukusanya maoni ya katiba mpya lakini kikubwa ni kwamba wananchi wengi hasa sisi wa maeneo ya pembezoni hatuielewi katiba na hata kujitokeza kwenye mchakato wa kutoa maoni kwakweli itakuwa vigumu kwani hatujui mahali ambapo panahitaji marekebisho,” alisema Mbise.
Kutokana na hali hiyo wananchi hao waliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutoa elimu ya katiba kwa wananchi hususani wa maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na kuwagawia vitabu vyenye muundo wa katiba au nakala za katiba, hatua ambayo itawapa uelewa na kuwapa fursa ya kushiriki zoezsi hilo muhimu katika nchi.
“Ili kufanikisha zoeszi hili la mabadioliko ya katiba, wananchi tuelimishwe kwa kina, lakini pia tulisikia kuna vitabu vya katiba lakini kama binafsi nilivyosikia vitabu hivyo ni vichache na si dhani kama vinaweza kuwafikia wananchi wote hapa nchini, lakini tunaomba vitabu hivyo vielekezwe zaidi vijijini, ambako hakuna uelewa wa katiba, ili kuweza kutoa fursa kwa wananchi wote kushiriki katika zoezi hilo la mabadiliko ya katiba,” alisema.
Naye Eliah Lukumai alisisitiza kutolewa kwa elimu ya katiba vijijini na kuongeza kuwa tume iliyoundwa ihakikishe inawafikia wananchi wote hususani maeneo ya vijijini ambako kuna wananchi wengi wenye shida na maskini bila kuangali ewezo wa kielimu wala kifedha.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Siha, Annarose Nyamubi alisema itakua ni changamoto kwa wananchi kuchangia maoni ya katiba ili hali katiba hawaifahamu hivyo ni vema nakala za katiba zikasambazwa kwa wananchi wote ili kutoa fursa kwa wananchi wote kutoa maoni yao.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Siha, Rashid Kitambulio alisema tayari nakala za katiba zimegawanywa abapo kila kijiji kimepewa nakala Tano na kwamba kwa sasa wataangalia uwezekano wa kuongeza nakala nyingine Tano kwa kila kijiji ili kuwezesha wananchi wote kufikiwa na nakala hizo na kuzisoma.
Wananchi hao walitochangamoto hiyo mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama kuwataka kujitokeza kwa wingi kutoa maoni ya mabadiliko ya katiba pindi tume itakapotoa ratiba na kuwafikia ili kuhakikisha inapatikana katiba ya wananchi wote na si wachache.