Wananchi Mara waogopa kuhesabiwa, wadai ni kifo

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Sensa, Dk. Albina Chuwa akisisitiza jambo

Na Thomas Dominick, Musoma

WANANCHI wa Mkoa wa Mara wametakiwa kuondokana na mila potofu ambazo zinadai kuwa mtu akihesabiwa basi anakufa au mwanamke hazai tena, badala yake kutoa ushirikiano na makarani wa Sensa inayotarajia kufanyika Agosti 26 mwaka huu nchi mzima ili Serikali iweze kuharakisha maendeleo yao baada ya kupata takwimu sahihi.

Rai hiyo ilitolewa na Mratibu wa Sensa Mkoa huo, Ramadhani Mbega baada ya kuwepo na madai ya baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Tarime kudai kuwa sensa sio nzuri kwa mujibu wa mila na desturi zao.

“Ni kweli kuna uvumi huo lakini kitu ambacho napenda kuwaambia wakazi wa Mkoa huu hasa wakazi wa Tarime lengo la kuhesabu watu ni kwa ajili ya serikali kupata idadi ya watu wake ili kuweza kupanga kwa urahisi na kuharakisha maendeleo ya wananchi wake,” alisema Mbega.

Alisema kuwa tayari zimeshaundwa kamati kwa ajili ya kutoa elimu na kuwahamaisha na kuwaelimisha wananchi kwa njia mbalimbali katika maeneo hayo umuhimu wa sensa kwa taifa na kuachana na uvumi ambao hauna maana na hausaidii juhudi za Taifa kupunguza umasikini kwa wananchi wake.

Mbega alisema kuwa sensa ya mwaka huu itahakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga, kutekeleza na kutathimini mipango mbalimbali ya maendeleo na sera kama vile MKUKUTA kwa Tanzania bara na MKUZA kwa Tanzania Visiwani.

Alisema kuwa tayari ilishawahi serikali ilishafanyika sensa ya majaribio Oktoba 02, mwaka jana ambapo katika mkoa wa Mara sensa hiyo ilifanyika wilaya ya Tarime kata ya Matongo.

“Miongoni mwa sehemu iliyofanyika sensa ya majaribio ni wilaya ya Tarime ambayo bado kuna baadhi ya watu wanapotosha umma na sensa hii ya majaribio na uzoefu na mambo muhimu yaliyopatikana katika sensa ya majaribio nchini ndio yatakayotumika zaidi katika sensa ya watu na makazi mwezi Agosti mwaka huu,”alisema.