WANANCHI DONGE WAISHAURI CCM KUTAFUTA UFUMBUZI MGOGORO WA UCHIMBWAJI MCHANGA

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala (aliyesimama) akizungumza na wazee pamoja na wamiliki wa mashamba ya uchimbwaji wa mchanga katika jimbo la Donge Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR

BAADHI ya Wazee wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na wamiliki wa mashamba ya kuchimbwa rasilimali ya mchanga Jimbo la Donge Wilaya ya Kaskazini “B” wamekishauri Chama hicho kuingilia kati mgogoro wa serikali kuwazuia wananchi wasichimbe mchanga katika maeneo ya wilaya hiyo. Ushauri huo wameutoa kwa nyakati tofauti mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” katika kikao cha kutafuta suluhu ya kutatua mzozo huo huko Tawi la CCM la Donge Mbiji Unguja.

Mkaazi wa Kijiji hicho, Bw. Bakar Juma Nahoda alisema kitendo cha Serikali kuzuwazuia wananchi wasichimbe mchanga kwa baadhi ya maeneo huku serikali hiyo ikiruhusu na kusimamia zoezi hilo liendelee kwa malipo maalum katika maeneo mengine, hatua hiyo imehatarisha ajira za baadhi ya vijana na wananchi waliokuwa wakitegemea sekta hiyo kama eneo la kujipatia kipato.

Bw. Juma alifafanua kwamba baada ya serikali kuwakata wananchi wasiendelee kuchimba mchanga katika maeneo hayo kwa madai ya kuepuka uharibifu wa mazingira, lakini zoezi hilo liliendelea kwa njia nyingine ya kuchimbwa mchanga kwa gharama maalum ya fedha zinazoingia serikalini.

Alisema toka serikali ilipotangaza rasmi utaratibu wa kuchimbwa kwa rasilimali hiyo na kuweka ulinzi mkali kwa baadhi ya maeneo wananchi wengi wa jimbo la Donge na Vijiji vyake wamekuwa na changamoto za ukali wa maisha hivyo aliiomba CCM iingilie kati mgogoro huo kwa lengo la kuupatia ufumbuzi wa kudumu.
Naye Ibrahim Mohamed Khamis alisema mbali na tatizo hilo pia kumeibuka changamoto nyingine ya baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani kutumia mgogoro huo kujinufaisha kisiasa kwa kuwashawishi baadhi ya vijana warudishe kadi za CCM bila kujali athari za baadae zinazotokana na uamuzi huo.

Aidha ameituhumu Kamati iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa ajili ya kushughulikia mgogoro huo kuwa iliwapuuza wananchi na kushindwa kufuata ushauri wa Wazee wa CCM wa jimbo hilo waliotaka shughuli zote za uchimbaji wa mchanga katika eneo hilo zisitishwe hadi hapo itakapopatikana suluhu ya kudumu.

“ Kama kweli serikali ina nia safi ya kuzuia athari za mazingira zinazotokana na uchimbaji mchanga basi na wao wasingeendelea kusimamia uchimbaji wa mchanga kwa baadhi ya maeneo waliowaondosha wananchi.

Pia tunaamini CCM, serikali kuu na wananchi wakikaa meza moja kujadiliana juu ya suala hili basi kila upande utaridhika juu ya maamuzi yatakayopatikana hapo lakini yawe na suluhu ya kuwapatia wananchi sehemu nyingine ya ajira ya kujipatia kipato chetu cha kila siku.”, alisema Mohamed miongoni mwa wakaazi wa kijiji hicho.

Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “Mabodi” aliahidi kuyafanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa na Wazee pamoja na wamiliki wa mashamba yaliyozuiliwa kuchimbwa mchanga katika eneo hilo ili wananchi wapate haki zao huku eneo lililofanyiwa tathimini za kitaalamu juu ya uchimbwaji wa mchanga nalo libaki salama.

Nimesikia kwamba wapinzani tayari wameshajipenyeza katika mgogoro huu kwa kushawishi wananchi waigomee serikali, jambo ambalo sio sahihi kama kweli wana nia wangeonyesha njia ya kutatua jambo hili kupitia njia ya mazungumzo na sio kukuza mgogoro.”, alieleza Dkt. Mabodi na kuongeza kwamba serikali iliyopo madarakani Chini ya Dkt. Shein ipo makini na inajali na kuheshimu mawazo ya wananchi wote na mzozo huo utamalizika kwa amani hivi karibuni.

Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema alisema lengo la serikali sio kuwaumiza wananchi bali ni kuwaongoza katika mambo mema hasa ya maendeleo, hivyo waendelee kuvumilia wakati CCM ikitafuta ufumbuzi wa kudumu juu ya tatizo hilo. Hata hivyo Dkt. Mabodi katika Kikao hicho alifuatana na viongozi na wajumbe wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo Bi. Khadija Jabir.