Wanakijiji Tanangozi waneemeka na mradi wa MUVI


Mmoja wa wakulima wa nyanya Kijiji cha Tanangozi, Iringa.

Na William Macha, Tanangozi, Iringa

WAKULIMA wa nyanya kutoka Kijiji cha Tanangozi, Wilaya ya Iringa Vijini, wameusifu mradi wa nyanya uliofadhiliwa na Asasi ya Muungano wa Wajasiriamali Vijijini (MUVI), kuwa umeanza kuwaletea mafanikio dhidi yao.

Kauli hiyo imetolewa jana kijijini hapa na mmoja wa wakulima wa zao hilo, Bw. Mtokambali Ngimba ambaye anatoka katika kikundi cha ujasiriamali kiitwacho ‘Nguvukazi’ katika kujiji hicho kinachofadhiliwa na MUVI.

Bw. Ngimba alisema ushauri mzuri walioupata kutoka MUVI ndio umemwezesha kulima kitaalamu zaidi na sasa anatarajia kuvuna kwa kiasi kikubwa na kuuza kwa bei nzuri mazao yake.

“Kwa kweli MUVI imetufungulia mlango wa mafanikio, wametusaidia sana nilikuwa nikitegemea kulima kipindi cha masika pekee, lakini sasa nimelima kipindi cha kiangazi na natarajia kuvuna kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyokuwa wakati wa mvua,” alisema mkulima huyo wa nyanya.

Aidha Ngimba ameongeza kuwa MUVI imewasaidia katika kuunda vikundi mbalimbali vya ujasiriamali na tayari vimekwisha sajiliwa na vimeanza kufanya kazi. Katika Wilaya ya Iringa tayari vikundi 42 kutoka katika vijiji 14, ambapo mradi huu unafanya kazi vimeundwa na vimesajiliwa. Usajili huo unatoa mwanga kwa wajasiriamali kwani utawasaidia kuwa na sauti inayoweza kusikika katika ushawishi na utetezi.

Kupitia Vikundi wanachama wanaimarisha mawasiliano na wadau nje ya kikundi na pia na serikali kuanzia kijijini mpaka ngazi ya taifa.

Akifafanua zadi kuhusu vikundi, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wakulima wa nyanya Wilaya ya Iringa vijijini, Bw. Pascal Sichalwe amesema kila kikundi kina wanachama 50 ambao kwa pamoja wanatakiwa walipe ada ya kiingilio ambayo ni sh. 50,000.

Aidha Sichalwe amesema mwitikio wa vikundi ni mkubwa na tayari zaidi ya nusu wametoa kiasi hicho kwa ajili ya uendeshaji. Mradi unajihusisha na kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kuibua na kutekeleza ubunifu katika zao la nyanja za masoko, teknolojia na sera ili kuinua ufanisi katika minyororo ya thamani ya mazao ya nyanya na alizeti.

Hata hivyo, mradi pia unawaunganisha wajasiriamali kupitia vyama vyao, kuunda majukwaa na kuwajengea uwezo ili waweze kukopeshwa na taasisi za fedha hivyo kuwa na uwezo wa kumudu huduma za uwezeshaji zinazotolewa na soko la huduma.