Wanakijiji cha Mwanadilatu walalamikia uchimbaji mchanga

Mwanakijiji, Marko Nyaigana (kushoto) akiwa na baadhi ya wanakijiji wenzake wakati walipozungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Na Joachim Mushi

WANANCHI kutoka kijiji cha Mwanadilatu wamelalamikia kitendo cha uharibifu wa mazingira kinachofanywa na baadhi ya watu wanaochimba mchanga maeneo mbalimbali kijijini hapo.

Wakizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam kupitia kwa wawakilishi wa wananchi hao, Marko Nyaigana amesema kitendo cha kufanyika uharibifu wa mazingira eneo hilo kimepamba moto na sasa kinaharibu pia miundombinu.

Mwakilishi huyo amesema hivi sasa hali ni mbaya zaidi kwani magari ya kuchimba mchanga yameongezeka katika Kitongoji cha Langweni hivyo kubaki na mashimo makubwa ya mchanga yanayomilikiwa na kampuni mbalimbali za ujenzi kutoka Jijini Dar es Salaam.

“Kama hiyo haitoshi magari hayo yamekuwa hata yakiharibu barabara ambazo zilikuwa zinapitika kwa uraisi muda wote…baadhi ya madaraja yamebomoka na kuacha barabara hizo zikititia na kubaki mabonde matupu. Barabara ya kutoka Mbande kuja Yombo imeharibika na haipitiki kwa ajili ya shughuli hizo,” alisema Nyaigana.

Alisema waharibifu hao wamechimba mchanga hadi katika maeneo ambayo yalikuwa yakitumika kama njia za watembea kwa miguu na kuzifanya njia hizo kutopitika suala ambalo limeleta kero kubwa kwa wakazi anuai.

“Hivi sasa kila unapopita watu wanachimba mchanga…wamesababisha eneo zima la Kitongoji cha Langweni ambalo lilikuwa tambalale kuonekana lina mashimo yasio na msingi,” alisema mwakilishi huyo.

Aidha amesema hali hiyo ni hatari kwa sasa kwani endapo mvua zitaanza kunyesha huenda zikaleta maafa makubwa kutokana na uharibifu wa mazingira uliofanywa katika ardhi hiyo ya Kijiji hicho.

Wananchi hao wamewalalamikia viongozi wa Kitongoji hicho kwa kuuza maeneo ambayo yametengwa na wakazi hao kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na yale ya wazi na sasa yanafanyiwa uchimbaji wa mchanga tofauti na makubaliano.

Hata hivyo wamedai mwenyekiti na Mtendaji wa Kitongoji cha Lengwani wamekuwa wakikusanya mapato kwa miezi minne mfululizo sasa na hakuna mwananchi anayejua kuna fedha kiasi gani ambazo zimetokana na shughuli hiyo. Viongozi hao pia wamekuwa wakijichukulia maamuzi wenyewe hivyo kuendeleza mgogoro juu ya suala hilo.