Wanajeshi wadaiwa kuvamia kijiji Dar

Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange

TAARIFA zilizotufikia jana majira ya saa nne asubuhi kutoka nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ni kwamba; watu wanaodaiwa kuwa ni Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi nchini (JWTZ) wamevamia Kijiji cha Kimbiji. Taarifa zinasema wanajeshi hao walivamia na kuvunjiwa makazi yao pamoja na kuharibiwa mazao.

Chanzo cha habari cha mtandao huu kilisema, malori manne yaliyojaa wanajeshi yalikivamia Kijiji cha Kimbiji nje kidogo ya Dar-es-Salaam, na kuvunja vunja makazi ya wanakijiji hao.

Taarifa zinadai baadhi ya wanajeshi hao walichukua hadi baadhi ya vifaa vilivyojengewa makazi ya wanakijiji hao na kupakia kwenye magari yao na kuondoka navyo. Wanakijiji walipo jaribu kuuliza kulikoni walijibiwa kuwa hawarusiwi kukaa katika eneo hilo. Baadhi ya Wanajeshi walidai kuwa eneo hilo ni sehemu ya eneo la jeshi na ni
maalumu kwa shughuli za kulenga shabaha kwa askari hao.

Hata hivyo wanakijiji hao na uongozi wa Serikali ya Kijiji umesema hauna taarifa yoyote ya kisheria kutoka serikalini, kwamba Idara ya Ardhi, Ofisi ya Mkoa imekitoa Kijiji cha Kimbiji kwa wanajeshi.

Mpaka tunaenda mitamboni wanakijiji wa Kimbiji walionekana kuwa njia panda kwa kushindwa wahoji wapi juu ya tukio lililofanywa na walinzi hao wa nchi. Baadhi ya wanakijiji wameiomba Serikali kuingilia kati suala hili na pia kuvilaani vitendo vinavyofanywa na wanajeshi kwa
kuvamia makazi na kuaribu mali za wapiga kura.

Walisema hata eneo lao halimo katika mpango mpya wa kuuendeleza mji mpya wa Kigamboni, na kuwa kinacho fanywa na wanajeshi hao ni kujichukulia ardhi kimabavu jambo ambalo ni hatari. Juhudi za dev.kisakuzi.com kupata ufafanuzi kutoka kwa msemaji wa JWTZ hazikuzaa matunda. Mtandao huu unaendelea kuwatafuta wahusika.