WAKATI zimebaki siku nne kuanza kwa Bunge la Katiba kwa mujibu wa sheria, wanaharakati wamewataka wajumbe wa Bunge kuwa makini na kutunga kanuni ambazo hazitawanyima uhuru wa kupaaza sauti za makundi yote yaliyoko pembezoni.
Pamoja na hayo wamewataka wajumbe kuhakikisha rasimu ya tatu ya katiba ambayo italetwa kwa wananchi kupigiwa kura za maoni inabeba sauti za jamii nzima ikiwa ni pamoja na kuzungumnzia masuala ya huduma za jamii badala ya siasa pekee au muundo wa serikali.
Akitoa mada katika mjadala wa wazi katika viwanja vya TGNP Mtandao Mabibo Dar es salaam, mchambuzi wa masuala ya kijinsia Gema Akilimali amesema kuwa suala la Muungano lisitawale mjadala wa Bunge maaluma wala muundo wa serikali bali wajumbe wajikite katika kujadili ibara muhimu zinazozungumzia haki za msingi za binadamu na upatikanaji wa huduma za kijamii ambazo zilijadiliwa zaidi na wananchi wa kawaida wakati wa mchakato wa utoaji wa maoni na mabaraza ya katiba.
“wabunge wanaotoka kwenye makundi ya kijamii wajitahidi kusimama imara, wasihofu, wasitazame elimu za watu na vyeo bali wapambane kuhakikisha sauti zao zinakuwa na nguvu na zinaingia kwenye katiba mpya. Tunajua kuna changamoto ya uchache wa uwakilishi wa wananchi, wanasiasa ni wengi zaidi kwenye hili Bunge lakini kama wao wachache watasimama imara watashinda..”alisema Akilimali
Akilimali alisema kuwa Bunge linatakiwa kuendeshwa kwa siku 70 tu zilizopendekezwa kujadili rasimu yote na kutoa maoni na sio kuomba nyongeza ya siku zaidi au kukimbilia kuwa siku 90.
Naye mwanaharakati Asseny Muro alisema kuwa Bunge linapaswa kuheshimu maoni ya wananchi na wakati likiendelea Dodoma wajumbe wasifungwe kusikiliza sauti zilizopo nje ya Bunge ambazo wanaharakati watakuwa wakiendelea kuzipaaza.
“Tunapinga kabisa mfumo wa kura za ‘ndio’ au ‘sio’ tunataka kila kifungu kitakachojadiliwa kipitishwe kwa kura za kidemokrasia ambazo zitawafanya wote kushiriki kikamilifu na kuwa huru. Tunapendekeza kura za siri za kuandika”alisema Muro
Washiriki hao wa mdajala wa kila Jumatano unaoendeshwa na TGNP walisema kuwa wabunge watakapo kaa na kutunga kanuni za kuliendesha wazingatie haki za wananchi walio nje ya Bunge ambao wanapaswa kuendela kujadili na kutoa maoni yao kwani Mchakato wa kushuirikisha wananchi haujafungwa nab ado Bunge ni chombo cha wananchi.
Aidha wamesema kuwa uongozi wa Bunge utakaochanguliwa unapaswa kuheshimu sauti za wote bila kubagua kwa minajili ya itikadi za kichama, kidini, kikanda au kikabila.