Wanaharakati wataka Dk Mponda, Lucy Nkya wajiuzulu

Wanaharakati wakiandamana na kufunga barabara kushinikiza Serikali itatue mgomo wa madaktari hivi karibuni

Na Joachim Mushi

TAASISI kadhaa nchini ambazo zinapigania haki mbalimbali za jamii na usawa zimemtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Haji Mponda na Naibu wake, Lucy Nkya kujiuzulu mara moja kwa kile kushindwa kutatua mgogoro wa madaktari na kusababisha vifo na madhara makubwa kwa Watanzania.

Kauli hiyo ya pamoja imetolewa leo jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na muungano wa vyama hivyo, huku vikisisitiza kuwa kama viongozi hao watagoma kujiuzulu basi Rais Jakaya Kikwete kuingilia na kuwafukuza kazi haraka viongozi hao.

Taasisi na vyama vilivyotoa kauli hiyo ni pamoja na Policy Forum, Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), SIKIKA, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), taasisi ya HAKIARDHI, taasisi ya HAKIELIMU, GDSS, Jipange, ForDia na FemAct.

Taasisi hizo pia zimemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuutangazia umma, ndani ya wiki moja hasara na madhara ambayo wameyapata wananchi na Taifa kwa kipindi chote cha mgogoro na madaktari.

Aidha wamemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kuomba radhi kwa uma kwa kile kuonesha kauli za kibabe bungeni kwa kuzima hoja za wabunge kutafakari mgogoro huu, huku akijua kufanya hivyo ni kuendeleza maafa yaliyokuwa yanayowakumba Watanzania.

Wameitaka tume iliyounda kushughulikia tatizo hilo itoe taarifa zake kwa umma kila mwezi ili wananchi waweze kufuatilia utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali na madaktari.

“…Kutokana na mgogoro huu wa madaktari Serikali ijifunze kuchukuwa hatua mara moja kila linapotokea tatizo ili kuepusha madhara yeyote,” wamesema wanaharakati hao katika taarifa yao kwa vyombo vya habari.

Hata hivyo wamewashukuru madaktari kwa kurudi kazini leo kwani wamebaini hospitali zote za umma mkoani Dar es salaam zinaendelea kutoa huduma baada ya kuzitembelea. “Tunawaomba sana muendelee kuwahudumia wananchi kwa moyo wote na linapotokea tatizo meza ya majadiliano itumike ili kuepusha madhara kama tulivyoshuhudia kwenye mgogoro huu,” imesema taarifa hiyo.

Pamoja na hayo wamezitaka mamlaka zote nchini kutambua, na kuheshimu uwajibikaji kwa wananchi walioziweka madarakani kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“…Ni vema tukakumbuka kuwa nchini duniani zimekuwa na tabia ya kuwashikilia, kuwashitaki na kuwatishia watetezi wa haki za binadamu kwa tuhuma zisizo na msingi ili kuendeleza unyanyasaji na ukandamizaji. Serikali itambue kuwa pale Serikali zilipokuwa zikijikita kwenye tabia hizi kandamizi, ziliambulia kuongeza matatizo na hata kuishia kumwaga damu za watu wake na hata viongozi wenyewe. Wanaharakati tunaomba mshikamano na umoja kutoka kwa wananchi wote wenye uchungu na mapenzi mema kwa taifa letu.” Imemalizia taarifa hiyo.

Wakizungumzia madhara yaliotokana na mgomo wa madaktari pamoja na haki zilizovunjwa na wahusika, wamesema; mgogoro huu umevunja haki ya kuishi kwa wananchi kadhaa na umehatarisha haki za raia wengi sana; inakadiriwa kuwa wananchi wengi wamekufa kwa kipindi hiki cha mgogoro huku wengi zaidi wakipata madhara yasiyorekebishika na huku maelfu wakiteseka na maumivu makali.

Pia Serikali imeonesha udhaifu mkubwa katika kutumia mamlaka iliyopewa na wananchi, hususani wajibu wake wa kusimamia haki za binadamu;ikiwa ni pamoja na kutotoa maamuzi sahihi na kwa wakati na hivyo kusababisha madhara makubwa kwa jamii.

“Serikali imeshindwa kutumia rasilimali tulizoikabidhi, kutatua tatizo hili huku ikifumbia macho matumizi mabaya na makubwa ya fedha za umma ya maafisa na viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Aidha viongozi wa Wizara hii wameshindwa kabisa kutoa uongozi stahiki kwa watendaji na madaktari ambao ndio watekelezaji na watoa huduma kwa jamii,”

“Katiba inatoa jukumu la moja kwa moja kwa wananchi kuchukuwa hatua za kuiwajibisha Serikali kutekeleza wajibu wake;na kwamba,pale wananchi tulipochukua jukumu la kuikumbusha Serikali wajibu wake na kuitaka kuchukuwa hatua stahiki na za haraka kutatua matatizo haya, Serikali imechukuwa uamuzi wa kutumia mabavu kutukamata na kututisha.Siyo tu kuwa hii haikubaliki lakini pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” imesema taarifa yao.