Na Mwandishi Wetu
WANAHARAKATI kutoka sehemu mbalimbali wametoa rai kwa Rais Jakaya Kikwete kulivunja Bunge maalum la
Katiba ili kuunda Bunge huru litakalokuwa na wawakilishi wasio wabunge wa Bunge la kawaida. Wanaharakati hao kutoka vikundi mbalimbali vya kijamii na asasi za kiraia wamefikia uamuzi huo leo jioni katika kusanyiko lao la kila Jumatano la Semina za Maendeleo na Jinsia (GDSS) katika viwanja vya TGNP Mabibo, walimtaka Rais Jakaya Kikwete kulivunja Bunge hilo ili litakaporudi Dodoma Agosti mwaka huu liwe na timu ya watu wachache watakaofanya kazi ya kutengeneza katiba nzuri ya wananchi na kwa muda unaotakiwa.
Bunge la Katiba linaahirishwa wiki iliyopita kupisha Bunge la Bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015, likiwa limetumia gharama ya karibia billion 27, za walipa kodi kwa mujibu wa Waziri wa Fedha Bi. Saada Mkuya. Ndani ya siku 67. Kwa muda wote huo Bunge hilo limekaa kujadili Rasimu ya pili ya Katiba, haijaweza kupitisha hata ibara moja, kati ya ibara 240.
Akizungumza mwezeshaji mkuu wa semina hiyo, Badi Darus alisema kuwa wao kama wanaharakati waliamua kuunda kamati ambayo inaongoza mijadala hiyo ambayo katika uchambuzi wao wamekuja na mapendekezo ya kuwa Bunge maalum la katiba livunjwe na serikali isitenge fedha zaidi kwenye Bunge hilo.
“Tunapendekeza kuwa Bunge la katiba livunjwe, fedha za walipa kodi siziendelee kutumika vibaya kuwalipa wabunge ambao mwisho hawataleta katiba ya wananchi. Tunataka Katiba ya wananchi lakini wao wametumia muda waliopewa kugawanyika kimakundi na kuwatisha wananchi kuwa katiba ikipita kama ilivyo rasimu ya pili jeshi litachukua nchi. Sisi tumeona kuwa haya na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, watu hawana maji, dawa, wala vitabu mashuleni, fedha hizo ziende kwenye sekta hizi,” alisema Darus.
Darus alisema kuwa wananchi walianza kukata tamaa baada ya wabunge kuanza kutumia muda mwingi kutukanana matusi, kukejeli kazi ya Tume ya mabadiliko ya katiba, kuzungumza masuala binafsi badala ya rasimu ya wananchi. Akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi alisema kuwa kunahitajika usuluhishi wa harakati wa makundi yaliyoibuka Bungeni ili kutafuta maridhiano na kuweza kuwaweka pamoja wananchi kama kweli tunataka kuwa na katiba mpya ya wananchi.
“sote tunaona tayari kuna makundi makubwa yanayokinzana, na baadhi hawapo ndani ya Bunge maalum la katiba, lakini hatuwezi kupata Katiba mpya kama hakuna maelewano, makubaliano na kuvumiliana kwa manufaa ya taifa hili, tunahitaji maridhiano ya dhati na kila upande ukubali kuwa kazi inayofanyika ni kwa ajili ya watanzania wote wa vijijini na mijini…”alisema Liundi.
Kwa upande wake Filibert Kilango alisema kuwa kamati yao inawakilisha wananchi wote ambao ni wana GDSS wanaoshiriki semina hizo na kila mara itajitahidi kufuatilia mchakato wa katiba mpya na kutoa taarifa kwa wananchi pale ambapo mambo hayaendi vizuri.
“sisi kamati ya GDSS tunachoona kama wanaharakati tunahitaji kuunganisha nguvu na kufanya kazi ya ziada ya kuwahabarisha wananchi. Jiwe la msingi la maendeleo ni usawa wa kijinsia, wanasiasa wameanza mjadala masuala ya msingi ya wananchi hayakufanyiwa kazi, sauti zetu sasa ni lazima kuzipaaza wenyewe” aliongeza Kilango.
Bunge la Katiba linaahirishwa hii leo kupisha Bunge la Bajeti, likiwa limetumia gharama ya karibia billion 27, za walipa kodi kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Bi. Saada Mkuya. Ndani ya siku 67 ambayo Bunge hilo limekaa kujadili Rasimu ya pili ya Katiba, haijaweza kupitisha hata ibara moja, kati ya ibara 240. Bunge maalum la katiba litaendelea tena August 5 mwaka huu baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge la bajeti na haijatangazwa kama limepewa siku ngapi.