Wanaharakati wa mazingira Afrika Mashariki wapewa changamoto

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Na Nicodemus Ikonko, EANA-Arusha

MSAJILI wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), Dk. John Ruhangisa ametoa changamoto kwa wanaharakati na watetezi wa mazingira kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote anayetishia uharibifu wa mazingira katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Akihutubua wandishi wa habari muda mfupi baada ya Kitengo cha Rufaa cha EACJ kuthibitisha kwamba mahakama hiyo ya kanda inayo mamlaka ya kusikiliza migogoro inayohusiana na masuala ya mazingira Machi 15, 2012, Dk. Ruhangisa alisema; “uamuzi wa mahakama ni ujumbe wazi kwamba wananchi wa kanda hii hawana sababu ya kufumbia macho kuvunjwa kwa haki za kulinda mazingira yao.’’

Mapema EACJ ilitoa amri ya kuizuia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kujenga barabara kuu kupitia ndani ya hifadhi kongwe ya taifa ya Serengeti kufuatia shauri liliofunguliwa na taasisi moja ya Kenya, ijulikanayo kama the Africa Network for Animal Welfare (ANAW) ikidai kwamba ujenzi wa barabara hiyo utaleta madhara kwa wanyama.

Lakini Serikali ya Tanzania ilikata rufaa kupinga hatua hiyo ya ANAW kwa maelezo kwamba, EACJ haina mamlaka ya kusikiliza mashauri yanayohusiana na masuala ya mazingira.

“Hatusiti hata kidogo kubaini kwamba vifungu vingi vya Mkataba wa EAC vimeonyesha wazi na kwa pamoja kutoa mamlaka kwa EACJ kushughulikia masuala ya migogoro ya mazingira,’’ inasomeka sehemu ya waraka wa hukumu hiyo yenye kurasa 26.

Kwa mujibu wa Dk. Ruhangisa, hukumu hiyo imetoa ufafanuzi juu ya suala muhimu linalogusa jamii moja kwa moja. “Inatoa changamoto kwa wananchi wakiwemo wanaharakati na watetezi wa mazingira kujitokeza kutetea masuala yanayohusu migogoro ya mazingira katika Afrika Mashariki kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki.’’

Alisisitiza zaidi kwamba ‘’tukiona uharibifu wa mazingira, Mahakama hii ina mamlaka ya kuyashughulikia. Kitengo cha Rufaa kimetueleza.’’

Alifafanua kwamba masuala ya mazingira hayajikiti tena kwenye nchi moja tu ndani ya kanda hiyo ya Afrika Mashariki yenye nchi tano ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

“Wanyama huhama kutoka Tanzania (hifadhi ya taifa ya Serengeti) katika msimu fulani kwenda Kenya na pia huhama toka Kenya (hifadhi ya taifa ya Maasai Mara) kuja Tanzania mara kwa mara. Hivyo uharibifu wowote utaziathiri nchi zote mbili,’’ Dk. Ruhangisa alitoa mfano.

Alisema pande zote zinazohusika katika mgogoro huo sasa ikiwa ni pamoja na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na upande wa mlalamikaji, ANAW, watajulishwa tarehe itakayopangwa kuanza kusilikizwa kwa shauri hilo.

Nayo Wakili wa ANAW, Saitabao Ole Kanchory aliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) katika mahojiano kwamba “nimefurahia uamuzi uliotolewa na mahakama na sasa nasubiri kwa hamu kusikilizwa kwa shauri hili.’’