WANAHARAKATI wa ngazi ya jamii na washiriki wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na TGNP Mtandao wametoa tamko huku wakiainisha dosari walizozibaini katika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni.
Akisoma tamko hilo leo jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari, Katibu wa Kamati ya uchambuzi wa rasimu hiyo, Esther William ameshauri rasimu ibadilishe sifa ya kiwango cha elimu ya mbunge kuwa kidato cha nne na kupinga mawaziri wasiwe wabunge ili kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa mihimili yote.
Akifafanua zaidi alisema Ibara ya 135 (b) ya Katiba inayopendekezwa imetamka sifa ya mbunge kuchaguliwa awe anajua kusoma na kuandika Kiswahili au kingereza suala ambalo likipitishwa linaweza kudidimiza maendeleo ya taifa kwani bunge linatakiwa kupitia na kuchambua kwa kina mikataba mbalimbali ambayo kwa sehemu kubwa ipo kwenye lugha ya kingereza.
Alisema ndani ya Katiba inayopendekezwa Ibara ya 111 kifungu cha (1) (d) imetaja sifa ya kuwa waziri au Naibu Waziri kuwa ni lazima awe ni mbunge, jambo ambalo alidai kifungu hicho kinaendeleza mgongano wa madaraka kati mihili mikuu miwili ya dola yaani Bunge na Serikali.
“…Tunadai mawaziri wasiwe miongoni mwa wabunge ili kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa mihimili yote mitatu kwa kila mhimili kujitegemea,” alisema Bi. William.
Aidha tamko hilo ambalo pia limesainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, TGNP Mtandao Lilian Liundi limetaka suala la uwiano wa 50/50 katika nafasi na ngazi zote za maamuzi kati ya wanawake na wanaume kuanzia ngazi za chini kabisa hadi taifa, litamkwe wazi ili kuondoa utata, ikiwa ni pamoja na rasimu kuweka ukomo wa vipindi vya kugombea kwa wabunge na mfumo mzuri wa kuwawajibisha viongozi wasiotimiza majukumu yao kwa wananchi.
Alisema haki ya kupata maji safi na salama iwe ni haki ya kikatiba ili kuweza kuwapunguzia wanawake mzigo wa kutembea umbali mrefu wa kutafuta maji na kushauri kuwekwa mfumo mzuri wa kuwasaidia makundi ya walio pembezoni kuweza kupata huduma bora za afya bila ya kikwazo.
“…Tunadai kipengele cha ukomo kwa wawekezaji kutumia ardhi ili kuweza kuepusha migongano na migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji katika suala zima la umiliki wa ardhi….katiba iunde chombo maaalum kitakachosimamia haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi,” alisema.
Kamati hiyo ya uchambuzi pia ilipendekeza rasimu ya katiba kutambua haki ya kupata elimu kutoka elimu ya awali hadi kidato cha nne ili kuweza kuondoa matabaka katika jamii na sio kuweka utaratibu tu wa upatikanaji wa elimu, ikiwa ni pamoja na kufuta kipengele cha Benki kuu ya Tanzania (BOT) kutowajibishwa na kudhibitiwa na mtu au mamlaka yoyote ya kiutendaji ili kuimarisha mfumo wa uwajibikaji.
“…Ibara ya 257 kifungu cha (3) kimetoa uhuru kwa Benki kuu ya Tanzania (BOT) kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiliwa, kudhibitiwa au kupewa maelekezo na mtu au mamlaka yoyote. Kifungu hiki kinakinzana na dhana bora ya uwajibikaji na utawala bora na kinatoa mwanya wa ubadhirifu na matumizi ya mabaya ya fedha za umma kwa kigezo cha watendaji wa benki kuu kutowajibishwa…” alisema Bi. William.