WAANDISHI wa Habari wametakiwa kuwa msatari wa mbele katika kuandika Habari za uhamasishaji juu ya umuhimu wa Uwekezaji hapa Nchini ili kuweza kuongezeka kwa ajira za Wananchi kutoka katika Makampuni na Wawekezaji mbalimbali watakaokuja Kuwekeza shughuli za Kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji Dk. Mary Nagu alipokuwa akifungua Kongamano la kutoa fursa za Uwekezaji Mkoani Mara lililoandaliwa na Taasisi ya MEEDA Kwa kushirikiana na Chuo cha Utafiti cha Sweeden (SWEACC) katika ukumbi wa mikutano wa Hotel ya Afrux Mjini Musoma.
Waziri Nagu alisema Mkoa wa Mara unazo fursa nyingi za Uwekezaji hivyo Waandishi wakitumia nafasi waliyonayo kuzitangaza kutawafanya Wawekezaji mbalimblai kuja Kuwekeza na kupelekea kutoa nafasi ya kuongezeka kwa ajira na kuongeza kipato kwa Wananchi kutokana na kuongezeka kwa Makampuni na hivyo kuongezeka kwa shughuli za Maendeleo.
Alisema Nchi haiwezi kuendelea bila kuwa na Wawekekezaji kutoka katika Mataifa yaliyoendelea na kudai kuwa hata hayo Mataifa yanayoendelea yalipokea Wawekezaji katika Nchi zao na leo hii yameendelea hivyo kuomba kupewa ushirikiano kwa Wawekezaji watakao kuja kuwekeza ili kuweza kuharakisha Maendeleo kwa Wananchi.
Waziri huyo wa Uwekezaji na Uwezeshaji ameipongeza Taasisi hiyo ya MEEDA kwa kuandaa Kongamano hilo ambalo limewakutanisha Wadau mbalimbali kutoka hapa Nchini na nje ya Nchi kwa kuwa utakuwa ni mwanzo mzuri wa kuwahamasisha Wawekezaji kuja kuwekeza katika Mkoa wa Mara na kuzitaka Taasisi nyingine kuiga mfano huo.
Alisema alipopata taarifa ya kushiriki katika Kongamano hilo alijisikia furaha kwa kupata nafasi ya kukutana na wadau mbalimbali wa shughuli za Uwekezaji kwa kuwa ndio mahala sahihi pakuweza kuzungumza nao na kueleza umuhimu wa Uwekezaji katika kuchangia shughuli za maendeleo hapa Nchini.
Awali akimkaribisha Waziri Nagu, Mwenyekiti wa Taasisi ya MEEDA ambao ni muungano wa watu wa Mkoa wa Mara wanaotaka kujikwamua kutoka kwenye umasikini Silivanus Chacha alisema lengo la kuandaa Kongamano hilo kwa siku tatu ni kueleza Fursa zilizopo za Uwekezaji ambazo zikihamasishwa kwa pamoja zitaongeza ajira kwa wakazi wa Mkoa wa Mara na kujikwamua kiuchumi.
Alisema kuwa tayari Wafanyabiashara watafiti kutoka Nchini Sweeden walishafanya Utafiti na kuona Mkoa wa Mara unazo fursa nyingi za Uwekezaji ambazzo zikitumiwa zitatoa nafasi ya kuongezeka kwa ajira kwa Wananchi wake hivyo kujikomboa kutoka katika tatizo la ajira na umasikini.
Chacha alisema kuwa lengo lingine la MEEDA ni kuanzisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili kutoa ajira kwa vijana na kuanzisha benki ya kijamii itakayokuwa ikitoa mikopo kwa mashariti nafuu ili kuweza kusaidia kuondokana na umasikini kwa Wananchi wa Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla.
CHANZO: Binda News