Wanahabari wapigwa Msasa kuandika Habari za Afya

Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezi

Na Shomari Binda

MUUNGANO wa vilabu vya waandishi wa habari nchini UTPC, umenza kutoa mafunzo maalum kuandika habari za afya kwa waandishi wa habari katika Mikoa yote nchini.

Hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuandika habari za afya zilizofanyiwa utafiti wa kina kwa lengo la kuboresha sekta ya afya na kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii.

Mkurugenzi wa UTPC, Bw. Aboubakar karssan, ameyasema hayo mjini Musoma wakati wa mafunzo ya kwanza ya siku nne kuanza kutolewa nchini kwa waandishi wa habari mkoani Mara ikiwa ni sehemu ya utatuzi wa matatizo na kuibua changamoto zinazokabili utoaji wa huduma ya afya nchini.

Amesema kwa muda mrefu jamii imekuwa ikikabiliwa na sintofahamu juu ya kujikinga na maambukizi ya magonjwa hususani Ukimwi kutokana na waandishi nchini kutoandika habari ambazo zimefanyiwa utafiti wa kina ambao hautoi majibu ya namna ya kujikinga na maambukizi mapya.

Kwa sababu hiyo ametoa wito kwa wanahabari mkoani Mara kutumia vema nafasi ya mafunzo hayo kwa lengo la kuibua changamoto zinazokabili sekta ya afya hasa maeneo ya vijijini ili kuwezesha wananchi kutumia mbinu bora za kujikinga na Maradhi.

Kwa mujibu wa mwezeshaji wa mafunzo hayo Dk Ahmed Twaha,amesema takwimu za kiafya hususani katika maeneo ya vijijini zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaofika katika vituo vya afya ni wanawake na watoto hivyo wanahabari wanapaswa kuibua mbinu kadhaa ya kunusuru kundi hilo kwa kuripoti njia bora za kujikinga na maambukizi ya maradhi kama vile Ukimwi na Malaria.