Mshauri na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu akitoa mada inayohusu mchango wa vyombo vya habari katika kuhamasisha matumizi rafiki ya huduma za kuzuia VVU na Huduma za Afya ya Uzazi kwa Vijana wakati warsha ya siku tatu ya mradi mpya kuhamasisha Vijana kuhusu udhibiti wa Maambukizi mapya ya VVU iliyofanyika hivi karibu katika kituo cha Habari na Mawasiliano Sengerema, Mwanza chini ya mradi wa SHUGA unaoendeshwa kwa pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa UNICEF na UNESCO kwa kuzishirikisha redio jamii nchini.
Na Mwandishi Wetu Sengerema
Licha ya jitihada za serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kupambana na mambukizi ya Virusi Vya Ukimwi hapa nchini, baadhi ya madhehebu ya dini nchini yameelezwa kuchangia kukwamisha juhudi hizo kutokana na imani zao .
Hayo yameelezwa na washiriki wa mafunzo ya siku tatu kwa vyombo vya habari vya jamii Tanzania juu ya kuendesha mradi mpya wa SHUGA unaolenga kutumia vyombo vya habari kutoa elimu na hamasa kwa vijana kukabiliana na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.
Washiriki hao kutoka redio mbalimbali za jamii hapa nchini wamesema kuwa kumekuwa na baadhi ya viongozi wa dini ambao kwa namna moja au nyingine hawakubaliani na matumizi ya kondomu kama njia sahihi ya kuzuia sio tu maambukizi ya VVU bali pia magonjwa ya ngono na kama njia ya mpango wa uzazi kutokana na itikadi zao kidini kwa kile wanachokiita kuzuia mimba ni dhambi.
Baadhi ya waandishi wa Habari na Mameneja kutoka vituo mbalimbali vya redio za jamii walioshiriki warsha hiyo wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasishwa kwenye warsha hiyo.
Yamekuwepo pia madhehebu mengine ambayo yamediriki kuzuia watu wanaoishi na VVU kuachana na matumizi ya dawa za kupunguza makali ya VVU na badala yake maombi ndio njia pekee ya uponyaji jambo ambalo linaonekana kuwa imani potofu kwa sababu ya kuchanganya imani na utaalamu wa kisayansi uliofanyiwa utafiti wa kina na sahihi.
Matokeo yaliyotajwa na washiriki baada ya ushawishi huo wa imani za kidini kwa watu wanaoishi na VVU kuacha matumizi ya dawa zenye kupunguza makali ya virusi ni kudhoofika kwa haraka, kushambuliwa na magonjwa nyemelezi yanayosababishwa na ukosefu wa kinga mwilini na hatimaye kufa.
“Dini ina nguvu kubwa katika kukuza maadili ya kawaida hasa juu ya heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu, upendo, huruma na uvumilivu na ina mengi ya kuchangia katika mapambano dhidi ya VVU / UKIMWI hususan huduma za kujitolea na kutoa sadaka kuwasaidia waliopatwa na maambukizi na walioathirika, kuhamasisha watu na makundi mbalimbali kwa kutumia maeneo ya maombi na kuchangisha rasilimali kwa ajili ya kuwajengea vituo vya malezi watoto, wagane na wajane ni muhimu kwa waandishi wa habari kuzitangaza na kuzipa umuhimu wake”.
Majadiliano hayo yalitokea baada ya mwezeshaji Bi. Rose Haji Mwalimu kuwasilisha mada yake iliyohusu ‘Mchango Wa Vyombo Vya Habari Katika Kuhamasisha Matumizi Rafiki Ya Huduma Za Kuzuia Maambukiziya VVU,’ na kusisitiza kwamba hadi sasa bado hakuna chanjo wala tiba sahihi kutibu VVU na UKIMWI. Njia sahihi ni kuzingatia na kufuata maagizo ya kitaalam katika kuthibiti na kupunguza maambukizi mapya hasa kwa vijana hususan matumizi ya kondomu.
Wakati huo huo waandishi wa habari wamehimizwa kuzingatia maadili na lugha mahsusi katika kuandika habari zinazohusiana na VVU pamoja na watu wanaoishi na VVU na kuacha kuandika habari ambazo zina mwanga mdogo, ni za mfumodume, kejeli, na zinakosa ujumbe mpya.
Mshauri na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu akiendelea kuwapiga msasa Mameneja na waandishi wa Habari kutoka redio za jamii zinazoshiriki mradi mpya wa SHUGA.
“Kuna changamoto kubwa katika kuandika na kutayarisha vipindi vya VVU kwa sababu mara nyingi lugha zinazotumika katika taarifa au zinanyanyapaa, kubagua, kuhukumu na kulaumu, vyombo vya habari havitendi haki”, alisema Bi Rose Haji Mwalimu ambaye ni Mshauri na Mkufunzi wa Redio Jamii nchini kutoka UNESCO katika warsha hiyo.
Warsha hiyo ya siku tatu imefanyika katika kituo cha Habari na Mawasiliano Sengerema, Mwanza chini ya mradi wa SHUGA unaoendeshwa kwa pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa UNICEF na UNESCO kwa kuzishirikisha redio jamii nchini.
Mshiriki wa warsha ya siku tatu ya mradi mpya kuhamasisha Vijana kuhusu udhibiti wa Maambukizi mapya ya VVU ujulikanao kama SHUGA kutoka Sengerema FM Redio, Peter Marlesa (kushoto) na Mshauri na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu wakifutilia kwa umakini kazi zilizokuwa zikiwasilishwa na vikundi kazi.
Mmoja wa washiriki kutoka redio ya jamii FADECO ya wilayani Karagwe mkoani Kagera akiwasilisha kazi ya kikundi chake ya kutengeneza jedwali la Message Matrix mbele ya washiriki wenzake.
Afisa Mipango VVU/UKIMWI kutoka UNICEF, Bi. Alice Ijumbe akifuatilia jambo kwa umakini wakati wa warsha hiyo.
Meneja wa kituo cha Kahama FM Redio, Marco Mipawa (kulia) akimshukuru Mshauri na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu kwa kuwapiga msasa kupitia mradi wa SHUGA unaolenga kuhamasisha Vijana kuhusu udhibiti wa Maambukizi mapya ya VVU mara baada ya warsha hiyo ya siku tatu.