Na Shomari Binda, Musoma
WAANDISHI wa habari wametakiwa kujenga tabia ya kufuatilia bajeti na sera za halmashauri, ikiwa ni pamoja na kufuatilia miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri husika, ili kuona kama imetekelezwa kwa kiwango ikilinganisha na fedha zilizotengwa kutokana na bajeti husika. Rai hiyo ilitolewa leo na mwanaharakati, Robert Renatus, ambaye ni mwezeshaji kwenye semina ya mafunzo ya uchambuzi juu ya sera na fedha za serikali, namna zinavyofanya kazi katika maendeleo ya jamii.
Renatus alisema fedha nyingi za halmashauri zinazotengwa kwenye bajeti zimekuwa hazitumiki ipasavyo kwa miradi iliyokusudiwa, ikiwa ni pamoja na miradi mingine kutekelezwa chini ya kiwango huku fedha hizo zikiwa zimetokana na kodi ya wananchi. Mwanaharakati huyo alisema kuwa kwa jinsi hiyo ni wajibu wa waandishi wa habari kujenga tabia ya kufuatilia bajeti za halmashauri na kuzipitia kwa kina, ikiwa ni pamoja na kuona ilivyopangwa, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi yake.
“Waandishi wa habari mnapaswa kufuatilia na kuzisoma bajeti za halmashauri kwa kina ili muweze kufuatilia utekelezaji wake….nyinyi kalamu zenu ni kitu cha muhimu sana maana mtaibua vitu ambavyo vimefichika, mtajua mapato na matumizi, na pia mtafuatilia utekelezaji wa miradi,” alisema.
Katika masuala ya Kisera, Renatus alidai kuzijua Sera mbalimbali za mipango ya Kimaendeleo ndio itakuwa nafasi nzuri kwa Waandishi wa Habari kuweza kuweza kuifahamisha Jamii juu ya mipango ya kimaendeleo inayowahusu.
Alisema Wananchi wanawategemea sana Wandishi wa Habari katika kuwafikishia taarifa mbalimbali muhimu ili waweze kuzifahamu na kupata nafasi ya kuwahoji viongozi katika utekelezaji wake.
Wakichangia kwenye semina hiyo, waandishi wa habari walisema kuwa ufuatiliaji wa bajeti za halmashauri umekuwa mgumu, kutokana na baadhi ya wakurugenzi na maafisa mipango kukatalia makaburasha ya halmashauri kwa maelezo kuwa hizo ni nyara za serikali hazipaswi kupewa raia wa kawaida.
Pia walisema kuwa pia wamekuwa hawapati ushirikiano wa kutosha kutoka kwa madiwani, kwa sababu baadhi ya madiwani pia wamekuwa hawasomi makaburasha hayo na badala yake baada ya kupewa uyaweka makabatini.
Akijibu hoja hiyo, mwanaharakati huyo alisema kuwa makaburasha ya bajeti za halmashauri ni kitu cha wazi na hivyo, mwandishi wa habari anayo haki ya kupewa na kulipitia, ili aweze kujua kulichomo, ambapo atapata fursa ya kuanza kufuatilia utekelezaji wake.
Aidha alisema kuwa ushiriki wa wanahabari kushiriki katika mchakato wa bajeti ni mkubwa sana, kwani watajua dhana nzima ya bajeti, kujua mchakato sahihi wa uandaaji wa bajeti ya serikali, nani anayeshiriki katika mchakato huo, kujua uhalali wa vyanzo vya mapato, pamoja na kujua uhalali wa matumizi ya fedha za umma.
Aliongeza kuwa pia waandishi watajua thamani ya kulingana na miradi, kutoa elimu ya bajeti katika lugha sahihi kwa umma, kudhibiti mapato na matumizi kwa kuibua udhahifu katika utekelezaji wa bajeti na kutoa maoni na mapendekezo ya maboresho ya bajeti. Alisema kuwa pia mchakato mwingine kwa wanahabari ni kulinganisha ufanisi kati ya bajeti na bajeti, kuhusisha sera na bajeti pamoja vipaumbele vya taifa na kuboresha upatikanaji sahihi wa taarifa za bajeti na namna ya kuzitumia.
Habari hii kwa hisani ya Shomi B Blogu