SISI Wanataaluma ya Habari hapa nchini tumeamua kuungana pamoja. Lengo kubwa likiwa kusaidiana katika matatizo mbali mbali hasa ya kiafya. Muungano huu hasa umechagizwa na kuugua kwa baadhi ya wenzetu magonjwa sugu ikiwemo saratani.
Tumeungana wanataaluma kutoka vyombo vya habari mbalimbali yakiwemo magazeti, Televisheni, Radio na Blogu anuai. Tuko chini ya mwamvuli wa kampeni maalum iitwayo ‘Media Car Wash for Cancer’. Tumelenga kusaidiana kupitia kampeni hii kutimiza lengo letu.
Kama mnavyo fahamu, hivi sasa tuna wenzetu 3 wagonjwa na hali zao haziridhishi. Waandishi wa habari ambao tumekusudia kuwasaidia hivi sasa kutokana na ukubwa wa matatizo yao ni Bwana Adolf Simon Kivamwo, aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Sunday Observer na The Guardian, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Ukimwi, (AJAAT), ambaye ana kansa ya utumbo.
Mwingine ni Danstan Bahai ambaye ni Mwandishi wa gazeti la Nipashe ambaye amepooza upande mmoja na hivi sasa yupo nyumbani kwao Muheza.
Pamoja na Athumas Hamis, ambaye ni Mwajiriwa wa Gazeti la Habari Leo, ambaye amepooza kuanzia sehemu ya kiunoni mpaka chini. Hawa wana mahitaji mbalimbali, ikiwemo gharama za matibabu pamoja kujikimu. Wote hawana bima za afya.
Wanahabari hawa mtakubaliana nami kuwa ni mahiri ambao mchango wao kwenye sekta habari na utumishi wao kwa umma wa watanzania unajulikana. Ili kufanikisha hili tumeunda Kamati Maalum inayojumuisha wajumbe kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Lengo la kamati hii, ni kuchangisha fedha kwa ajili ya madhumuni hayo. Kabla ya kampeni hii tumekuwa tukiwasaidia kwa michango mbali mbali, lakini misaada yetu imekuwa ikipungua siku hadi siku, hivyo tumeona tuujulishe umma ili nao watuchangie. Kamati imeandaa harambee ya kuchangisha fedha kwa mtindo wa kuosha magari katika viwanja vya Leaders Club, siku ya Jumamosi Julai 4, 2015. Fedha zitazopatikana zitagawanywa miongoni mwa wenzetu hawa.
Aidha, kiasi kingine kitatumika kuwasaidia wanahabari wengine hususani wasioajiriwa ambao wangependa kujiunga na mifuko ya Bima ya afya nchini. Tunaomba Wadhamini mbali mbali wajitokeze kutuunga mkono katika kampeni hii. Akaunti ya Michango inapokelewa na kamati hii kupitia namba zifuatazo:
Tigo: 0653 155808
Voda: 0766 970240
Imetolewa na
Benjamin A.Thompson Kasenyenda
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi