Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum Vyuo Vikuu Waaswa

Mlau wa Mahafali ya nane ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaama (DUCE) Profesa Martha Qorro akizungumza wakati wa Mahafali hayo yaliyofanyika jana chuoni hapo. Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 1156 walitunukiwa Shahada na Stashahada za juu.

Mlau wa Mahafali ya nane ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaama (DUCE) Profesa Martha Qorro akizungumza wakati wa Mahafali hayo yaliyofanyika jana chuoni hapo. Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 1156 walitunukiwa Shahada na Stashahada za juu.

Wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma vyuo vikuu nchini wameaswa kutumia elimu wanayoipata kuendesha maisha yao ili waweze kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Prof. Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Kituo cha Stadi za Mawasiliano Martha Qorro ambaye alikuwa Mgeni Mashuhuri wakati wa Mahafali ya nane ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaama (DUCE) yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaaam.

Prof. Qorro alisema kuwa mwamko wa wanafunzi wenye mahitaji maalum kujiunga na elimu ya juu nchini ni mzuri licha ya changamoto zinazowakumba wanafunzi hao wanapokuwa chuoni.

“Hawa ni wanafunzi wenye uelewa mzuri wakipata mahitaji yao ya lazima yakiwemo fimbo nyeupe, vifaa vya kuandikia kwa kutumia nukta nundu, baiskeli za miguu mitatu, viti maalu na mahitaji mengine ya kijamii” alisema Prof.Qorro.

Prof.Qorro aliongeza kuwa ni wajibu wa vyuo vikuu nchini kikiwepo Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam kuwasisitiza kwa kuwauliza wanafunzi wanapojaza fomu za kujiunga waoneshe kuwa wanamahitaji maalum ili waandaliwe mahitaji hayo ikiwemo usafiri wa bajaji ndani ya chuo ili kuwawezesha kuwahi vipindi vyao katika maeneo mbalimbali ndani ya chuo.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) Profesa William Anganisye alipokuwa akitoa taarifa fupi kuhusu mafanikio chuo wakati wa Mahafali hayo alisema kuwa chuo hicho kimetimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake ambapo hadi sasa wamehitimu wanafunzi zaidi ya 8000 na jumla ya wahitimu 1156 walitunukiwa Shahada na Stashahada za juu katika mahafali hiyo ya nane.

Naye muhitim wa mwaka wa tatu katika ngazi ya shahada ya ualimu katika masomo ya sanaa Andrea Sanga ambaye pia ni mwanafunzi mwenye mahitaji maalum (mlemavu asiyeona) alisema kuwa mafanikio yake katika masomo yametokana na kuheshimu ratiba kuu ya masomo chuoni hapo pamoja na ratiba yake binafsi ya kujisomea.

Zaidi ya hayo, Sanga alisema kuwa maktaba ya chuo, ushirikiano mzuri kati yake na wanafunzi wenzake na walimu wake, kuhudhuria semina na kufanya kazi kwa wakati na kupunguza msongamano wa kazi nyingine ndiyo vimekuwa dira yake kuu ya mafanikio.