Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
WANAFUNZI wametakiwa kujiepusha na vitendo vitakavyochochea wao kupata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na mimba za utotoni jambo litakalowafanya wakatize masomo na hivyo kutotimiza ndoto za maisha yao.
Rai hiyo imetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari Mkonge iliyopo wilayani humo.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kuna baadhi ya wanafunzi wanajiingiza katika mapenzi kabla ya wakati kwa kufanya hivyo wanakumbana na mimba za utotoni na ugonjwa wa Ukimwi.
“Mimba na Ugonjwa wa Ukimwi vinapatikana kwa njia ya kufanya mapenzi yasiyo salama, msikubali kudanganywa na watu wazima ili muwe wapenzi wao watawaharibia maisha yenu.
“Sote tunajuwa kipindi cha balehe kinasumbua kijana anatamani kufanya kila kitu kilichopo mbele yake, epukeni majaribu haya! Mkiwa shuleni msifanye mapenzi wakati wake bado haujafika, msichana na mvulana mshirikiane katika masomo tu na siyo kufanya mapenzi,” alisema Mama Kikwete.
MNEC huyo aliwahimiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yao kwa kufanya hivyo wataweza kuepukana na ujinga, maradhi na umaskini.
Alisema, “Ili muweze kuwa na maendeleo ya elimu ni lazima muache utoro, msome kwa bidii, msome katika makundi ya watu wenye uelewa wa masomo tofauti wasiozidi saba pia nidhamu iwe msingi wa maisha yenu kwa kufanya hivyo mtafaulu.
“Wazazi wenu wamewasaidia kwa kuwapeleka shule, ukiwa na jitihada za makusudi utafanikiwa wekeni malengo katika maisha yenu, tengenezeni ratiba ya kujisomea nyumbani na walimu wenu wakiwapa mazoezi ya masomo mkafanye nyumbani mjitahidi kumaliza kwa wakati.”
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa wilaya ya Lindi ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Kilwa Abdallah Ulega aliwaambia wanafunzi hao kuwa wao ni viongozi lakini hadi wafike huko kuna milima na mabonde wanayotakiwa kuyavuka.
“Fanyeni jitihada katika masomo yenu kwani hakuna mtu aliyezaliwa na akili nyingi kuliko mwingine, ukiwa na akili ni jitihada zako binafsi, elimu ni vita lazima uishinde na hakuna mchawi katika masomo. Mkifanikiwa katika hili mtakuwa viongozi wazuri hapo baadaye,” alisema Ulega.
Naye Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi Mzee Alli Mtopa aliwasihi vijana hao kusoma kwa bidii ili waweze kuzitumia rasilimali zilizopo mkoani humo ikiwa ni pamoja na kufanya kazi za kitaalam katika sekta gesi kwani wasiposoma kazi hizo zitafanywa na watu wengine na wao watabaki kulalamika.
Akisoma taarifa ya shule, mkuu wa shule mwalimu Bahia Abubakar alisema shule hiyo yenye wanafunzi 643 wa kidato cha kwanza hadi cha nne na walimu 39 ilianzishwa mwaka 1966 ikiwa ni shule binafsi inayomilikiwa na watu wenye asili ya Asia lakini mwaka 1995 ilikabidhiwa kwa Serikali.
Alizitaja changamoto zinazowakabili ni upungufu wa walimu sita wa masomo ya sayansi na hisabati, uchakavu na upungufu wa majengo, utoro wa rejareja kwa wanafunzi, ukosefu wa uzio, upungufu wa samani na nyumba za walimu, wazazi kutoshiriki kikamilifu katika malezi na kuwahamasisha watoto kupenda shule.
Mwalimu Bahia alisema, “Mafanikio tuliyoyapata ni maendeleo ya taaluma yanaendelea kupanda mwaka hadi mwaka kwani matokeo ya kidato cha pili yamepanda kutoka asilimia 30.5 kwa mwaka 2011 hadi 90 kwa mwaka 2014 na matokeo ya kidato cha nne ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 35 kwa mwaka 2011 hadi 68 kwa mwaka 2014.
“Tumefanikiwa kuhamasisha wazazi kuchangia fedha kwa ajili ya kuwapatia wanafunzi uji shuleni na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa utoro wa rejareja pia juhudi zinaendelea ili kuwapatia chakula cha mchana, tunaendelea kutoa motisha kwa walimu ambao masomo yao yamefanya vizuri katika mitihani ya taifa na hatuna upungufu wa walimu wa masomo ya sanaa.”
Mama Kikwete aliwapa wanafunzi hao zawadi ya vifaa vya bendi ya shule, kutokana na tatizo la maji shuleni hapo aliahidi kuchimba kisima, aliahidi kuwapa wanafunzi mipira na jezi na kuwachangilia shilingi 1,670,000/= kwa ajili ya ziara ya masomo wilayani Bagamoyo.
Pia alikamilisha ahadi yake aliyoiahidi mwezi uliopita kwa shule ya Sekondari ya Angaza na kuwakabidhi wanafunzi pamoja na walimu vifaa vya bendi ya shule na mabati 100 ambayo yatatumika kuezeka chumba kimoja cha maabara kati ya maabara tatu zinazojengwa.
Wakati huo huo MNEC Mama Kikwete alitembelea tawi la Jamhuri na kuwataka viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi hilo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kuipigia kura katiba inayopendekezwa na kuwachagua viongozi wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.
“Katika wilaya yetu kila kata imepewa nakala za katiba inayopendekezwa 300 , tumieni muda wenu kuzisoma na kuelewa mambo yaliyoandikwa, wakati ukifika mkaipigie kura ya ndiyo kwani ni katiba bora kwakuwa imegusa maisha ya kila mtanzania,” alisisitiza Mama Kikwete.
Aidha aliwahimiza wajumbe hao kwenda Hospitali kupima saratani za tezi dume na shingo ya kizazi ili kama watakutwa na dalili za ugonjwa katika hatua za awali watatibiwa na kupona kabisa.
Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010. Hadi sasa ameshatembelea matawi yote 82 yaliyopo wilayani ya Lindi mjini.