Na Joachim Mushi, dev.kisakuzi.com- Mafinga
WANAFUNZI wenye ulemavu anuai katika Shule ya Msingi Makalala wameiomba
Serikali na wadau wengine kuwasaidia kuwajengea mazingira bora ya
kujifunzia kwa watoto wenye ulemavu ili waweze kupata elimu bora kama
ilivyo kwa watoto wengine.
Kauli hiyo imetolewa katika risala ya wanafunzi hao iliyosomwa jana
Wilayani Mafinga kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika
kiwilaya kwenye Shule ya Msingi Makalala nje kidogo ya Mjini wa Mafinga.
Katika maelezo yao watoto hao wameiomba Serikali na wadau wengine
kuwatizama kundi la watoto wenye ulemavu anuai kwa jicho la karibu, hasa
katika uboreshaji wa mazingira jumuishi ya kujifunzia katika shule zenye
watoto wenye ulemavu.
Pamoja na hayo wanafunzi hao walemavu wameomba kuboreshewa mazingira ya
lijifunzia katika Shule yao ya Makalala, ikiwa ni pamoja na kuwajengea
chumba maalumu kwa ajili ya kujifunzia kitakachokidhi mahitaji ya kundi
hilo maalumu.
Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Mafinga, Bi. Farida Mwasumilwe alisema licha ya Serikali
kujitahidi kuboresha huduma mbalimbali kwa watu wenye ulemavu bado kuna
changamoto nyingi hivyo kuomba wadau kushirikiana kwa pamoja kuwasaidia
watu wenye ulemavu hasa watoto.
Bi. Mwasumilwe aliwataka wadau mbalimbali kusaidiana kutoa elimu kwa baadhi
ya wazazi ambao bado wamekuwa na kasumba ya kuwaficha watoto wenye ulemavu
ndani hivyo kukosa haki za msingi ikiwemo elimu, ambayo ndio mkombozi pekee
kwa kundi hilo.
“Naomba tusaidiane kuwafichua watoto wote walemavu ambao baadhi ya wazazi
wamekuwa wakiwaficha ndani hivyo kukosa haki yao ya msingi. Pia jamii haina
budi kusaidia malezi ya watoto kwani mzigo huu sio waserikali pekee,”
alisema Mwasumilwe ambaye ni Ofisa wa Elimu Shule za Msingi Wilaya ya
Mafinga.
Katika maadhimisho hayo yalioambatana na michezo mbalimbali kwa makundi ya
watu wenye ulemavu, Shirika la Sightsavers limeahidi kumalizia ujenzi darasa la kisasa pamoja na baadhi ya vifaa vya kujifunzia litakalokuwa na uwezo wa kufundishia wanafunzi wenye ulemavu shuleni hapo.
Shirika hilo mbali na kukabidhi fimbo 35 maalumu za kutembelea kwa wanafunzi wasioona pia limeahidi kutoa gari la kisasa kwa shule ya Makalala ili kuwasaidia wanafunzi walemavu hasa wasioona kupata huduma zao nje ya kituo hicho pale inapohitajika. (kila fimbo moja ina thamani ya sh 50,000 za kitanzania).
Maadhimisho hayo yaliandaliwa na taasisi anuai zinazofanya kazi na watu wenye ulemavu, zikiwemo Chama cha wasioona Tanzania (TLB), Kituo cha Habari Kuhusu Walemavu nchini (ICD), Sightsavers, CCBRT, INUKA, SHIVYAWATA kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu inasema, “Haki za Watoto wenye Ulemavu; Ni Jukumu letu Kuzilinda, Kuziheshimu, Kuziendeleza na Kuzitimiza”.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa dev.kisakuzi.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Kituo cha Habari Kuhusu Walemavu Tanzania (ICD)