Na Mwandishi wa Daraja
MOJA ya changamoto inayowakabili wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kipagalo na Shule ya Msingi Mahulu, zilizopo Makte Njombe ni kutopata chakula cha mchana wakiwa shuleni.
Akizungumza na Shirika la Daraja, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kipagalo, Ayoub Honelo anaeleza kusikitika kwake kwa hali hiyo huku akieleza; “inaumiza sana kuona mwanafunzi wa bweni anapata mlo mmoja tu kwa siku, wakati ana tumia muda mwingi darasani na baadaye anahitaji muda mwingi wa kujisomea.
“Mwanafunzi akisha kula chakula cha usiku basi ni hadi tena usiku, wakati mwingine wanasinzia darasani kwa sababu ya njaa na hata wanapokosa kuwaadhibu ni kama kuwaonea tu” anasema mwalimu huyo.
Aidha, anaendelea kusema kuwa kuna kipindi wazazi na walimu walikutana na kujadili suala hilo na wakakubaliana kutoa mahindi katika kipindi cha mavuno, mwezi wa saba mwaka jana, lakini zoezi hilo liligonga mwamba kwa sababu wazazi baadaye walihisi walimu wana nia ya kuiba chakula chao
“Wazazi ni wazito sana hata kufuatilia maendeleo ya kitaaluma ya watoto, kufuatilia afya zao pia ni kazi, kwa kweli serikali ya kijiji inapaswa kufanya kitu na kuchukua uamuzi juu ya hili” anasema Honelo
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahulu, Estobery Kimetelo anaeleza kuwa sababu kubwa inayofanya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mahulu kutokula chakula cha mchana ni wazazi kushindwa kuchangia chakula kutokana na kutokuwa na nguvu za kuzalisha ziada.
Pamoja na hayo imeelezwa kuwa madarasa yaliyopo katika shule hiyo yamechakaa kiasi kwamba hayafai kutumiwa kwa kuhofia kuwadondokea wanafunzi wakati wowote. Hata hivyo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuanza ujenzi wa madarasa mapya