WAATHIRIKA wa tukio la moto katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kiislamu ya Ilala iliyoteketea kwa moto jana wameeleza mazingira ya moto ulivyotokea katika ajali hiyo ambayo imepoteza mali mbalimbali za wanafunzi pamoja na kuteketeza madarasa yao. Wakizungumza na dev.kisakuzi.com eneo la tukio mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Kamaria Mohamed anayesoma kidato cha kwanza alisema moto uliibuka majira ya saa tatu kasoro wakiwa wanajisomea katika darasa maalumu la masomo ya jioni.
Alisema moto huo ulianzia katika bweni wanalolala wanafunzi na baadaye kutapakaa kwa kasi katika madarasa mengine pamoja na majengo ya Shule hiyo inayomilikiwa na Taasisi ya Maendeleo ya Kiislamu (IDF). Mwanafunzi huyo alisema maada ya moto kuendelea kutapakaa walimu walianza kuwatoa wanafunzi nje huku wakiendelea kupambana kuuzima jambo ambalo lilikuwa gumu kutokana na kasi ta moto.
Mohamed alisema yeye pamoja na wanafunzi wenzake wa kidato cha kwanza hawakufanikiwa kutoa vitu vyao ambapo viliteketezwa kwa moto kabisa. “…Sisi hatukufanikiwa kutoa vitu vyetu viliungua kabisa bora wenzetu baadhi wa kidato cha nne wao walifanikiwa kuokoa baadhi ya vitu…sisi tulikimbilia nje kuomba msaada,” alieleza mwanafunzi huyo.
Mmoja wa viongozi wa Msikiti wa Taqwal uliopo jirani na Shule hiyo, Sheikh Othuman Zuber ambao walishuhudia tukio hilo alisema bado wamepigwa na butwaa namna moto huo ulivyoteketeza majengo ya shule kwa kasi huku wakishindwa kujua chanzo chake.
“…Kwa kweli hata siye tumebaki midomo wazi kwanza mazingira ya moto wenyewe yalivyotokea na namna ulivyotapakaa kwa kasi ndani ya muda mfupi baada ya kuuona. Umeme ulikuwa umezima maana LUKU iliisha hivyo kuna mtu alikwenda kununua LUKU kabla ya kurejea moto uliibuka, hatujui chanzo ni nini lakini hakukuwa na umeme muda huo,” alisema kiongozi huyo.
Alisema moto huo umeunguza majengo yote ya shule hiyo pamoja na vifaa mbalimbali vya wanafunzi na shule. Hata hivyo haukujeruhi wala kuua wanafunzi wa shule hiyo. dev.kisakuzi.com ilishuhudia viongozi mbalimbali wa kidini na serikali wakifika kutoa pole na kuangalia madhara yaliosababishwa na moto huo kwa hatua zaidi.
Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa tukio zima kwa kushirikiana na wataalamu anuai wa majanga ya ajali. Mwandishi wa habari hii alishuhudia baadhi ya maofisa wa Polisi wakichukua maelezo kutoka kwa mashuhuda na wahusika watukio hilo.